HATIMAYE shindano la kumsaka mrembo albino jijini Mwanza limefikia tamati baada ya Zawadi Dotto (17) kuibuka kidedea na kutawazwa kuwa mshindi katika shindano hilo baada ya kuwagaragaza wapinzani wake sita.
Shindano hilo lilifanyika juzi usiku jijini hapa huku likiwakutanisha wasichana saba wenye ualbino ili kumpata mshindi atakayewakilisha mkoa kitaifa.
Warembo hao ni Hajra Sadru, Furaha Elias, Zabibu Abdalah, Anthonia Mathias, Pendo Faustine na Asteria Christopher walionyesha madaha na ubunifu jukwaani wakisaka nafasi hiyo.
Hata hivyo, walioingia tatu bora katika mpambano huo ni Zawadi Dotto, Furaha Elias
na Hajra Sadru ambapo Dotto aliweza kung’ara zaidi na kuwaacha wawili hao.
“Kwakweli sikutarajia kama ningeweza kushinda taji hili, kwa sababu wote umewaona walivyo safi, mimi nakiri kuwa ni kudra za Mungu labda nitapambana kupigania haki za watu wa albino,” alisema Dotto.
Mlimbwende huyo alijinyakulia zawadi ya simu aina ya Solar5, kitita cha Sh 100,000 na godoro, huku mshindi wa pili, Hajra Furaha, akijinyakulia simu, godoro na Sh 80,000 na mshindi wa tatu akijinyakulia simu, godoro na Sh 50,000.