Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
Bondia Yusuf Changalawe ambaye ni nahodha wa kikosi cha Faru Weusi wa Ngorongoro, Yusuf Changalawe amefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Mandela yanayoendelea nchini Afrika Kusini.
Changalawe ametinga hatua hiyo baada ya jana kumchakaza mpinzani wake Abdelgawwad Orabi Salah kutoka Misri kwa points 5-0.
Hii ni mara ya pili mabondia hao kukutana, mara kwanza ilikuwa katika fainali ya kufuzu Olimpiki kwa Bara la Afrika 2023, zilizofanyika Dakar, Senegal ambapo Changalawe alipoteza fainali na kukosa nafasi ya kwanza kushiriki Olimpiki ya Paris 2024.
Kwa mujibu wa Rais wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT) Lukelo Willilo, Tanzania inawakilishwa na mabondia watano na hadi sasa wamebaki wawili ambao ni Changalawe na Azizi Chala waliopo katika hatua ya nusu fainali.
Amewataja mabondia waliotoka baada ya kupoteza mapambano yao juzi kuwa ni Ezra Paulo Mwanjwango na Abdallah Mfaume ‘Nachoka’.
Mashindano hayo mapya ya Mandela yatafikia tamati kwa michezo ya fainali Jumapili Aprili 21, 2024.