22.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, July 23, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga yaiangukia Simba

Hassan Ramadhani ‘Kessy’NA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

KATIKA kile kinachoonekana ni kusalimu amri kwa watani wa jadi, uongozi wa klabu ya soka ya Yanga  umeliandikia barua  Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kusaidia kuiomba Simba kuandika barua  ya kumruhusu mchezaji wake wa zamani, Hassan Ramadhani ‘Kessy’ kujiunga na timu hiyo.

Awali Simba iligomea kuandika barua ya kumruhusu mchezaji huyo hadi pale Yanga watakapoona umuhimu wa kuandika barua kwao kuomba kutoa ruhusa.

Msimamo wa Simba ulitokana na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kumbania mchezaji huyo hadi hapo atakapokuwa na barua kutoka klabu yake ya zamani ya Simba, ili aweze kucheza  michezo ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mkataba wa Kessy unamalizika Juni 30 mwaka huu, ili acheze Yanga inatakiwa kuwa na barua ya mchezaji kuruhusiwa kuondoka Simba.

Habari za uhakika kutoka Yanga zinadai kuwa uongozi wa klabu hiyo ulisalimu amri na kulazimika kuandika barua hiyo na kuipeleka TFF jana jioni, kutokana na kukabiliwa na mchezo mgumu Juni 28 dhidi ya TP Mazembe, baada ya kupoteza mchezo wa awali uliochezwa Juni 19 dhidi ya Mo Bejaia ya Algeria huku wachezaji watano wakipewa kadi zitakazowaweka nje katika mchezo huo.

“Kwa sasa hakuna beki wa pembeni  anayeweza kucheza kwa ustadi na kuhimili vishindo vya TP Mazembe kama si Kessy, hivyo inawalazimu kupambana ili kuhakikisha mchezaji huyo anacheza mchezo huo,” kilisema chanzo hicho.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Rais wa klabu ya Simba, Evans Aveva, alisema licha ya uzalendo alionao hatathubutu kuwa wa kwanza kuandika barua hiyo kabla ya Yanga kuandika.

“Hakuna haja ya kuanza kulalamikiana wakati hadi sasa hivi sijaona barua ya Yanga hapa ofisini kwangu, wanataka Simba ifanye nini kama si wao kuandika barua kwanza na sisi kujibu,” alihoji Aveva.

Aveva aliongeza kwamba, hadi Yanga waandike barua ndipo ijulikane kama watamruhusu mchezaji huyo kuendelea na timu hiyo au la.

“Hatuna tatizo na klabu yoyote na mashabiki wa soka wasiwe wepesi kuilaumu Simba wakati Yanga yenyewe inashindwa kufuata utaratibu,” alisema Aveva.

Pia Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya klabu hiyo, Zakaria Hanspope, alisikika akisema kwamba hataweza kuandika barua hiyo kabla ya Juni 30 mwaka huu.

Awali akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas, alisema hakukuwa na sababu ya klabu ya Simba kushindwa kuandika barua ili kuthibitisha kumwachia mchezaji huyo kujiunga na Yanga.

“Lilikuwa jambo la utaratibu kwamba Simba imwandikie barua Kessy ya kuthibitisha kumruhusu kujiunga na Yanga, kinachotokea sasa ni vita ya utani wa jadi kama ilivyokawaida yao,” alisema.

Wakati huo huo, taarifa kutoka  Yanga zilidai kwamba  mshambuliaji mpya wa timu hiyo Mzimbabwe , Obrey Chirwa, anatarajiwa kujiunga na wachezaji wenzake mjini Antalya, Uturuki leo katika Hoteli ya Rui ambapo timu hiyo imeweka kambi hadi Juni 25 mwaka huu ili kujiandaa na mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika  dhidi ya TP Mazembe.

“Chirwa alirejea  nchini baada ya mchezo dhidi ya Mo Bejaia ili  kushughulikia kibali cha kufanya kazi nchini, hivyo alitarajia kuondoka jana saa 11:00  usiku kujiunga na wachezaji wenzake Uturuki,”  ilisema taarifa ya Jerry Muro.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles