22.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga ishindwe yenyewe

yanga*Wafikia hoteli waliyopanga mikakati kumuua Mnyama Sept 26

*Wapanga kufanya bonge la ‘surprise’ Taifa Jumamosi

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga sasa washindwe wenyewe kuwamaliza watani wao wa jadi Simba kutokana na maandalizi kabambe wanayofanya kuelekea pambano lao la keshokutwa litakalofanyika katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Yanga wamejichimbia visiwani Pemba katika hoteli ya kifahari ya Misali Beach Resort, ambako wamechukua hoteli nzima na kuweka ulinzi wa uhakika ili kukwepa hujuma zinazoweza kujitokeza kabla ya pambano hilo.

Ili kujihakikishia usalama wa wachezaji wa kikosi hicho ambacho kilitua visiwani humo kikitokea nchini Mauritius ambako walicheza mechi yao ya awali ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Cercle de Joachim, Yanga wameweka walinzi wao wenyewe na kukataa kulindwa na polisi.

Yanga wameweka kambi yao nje ya mji Chake Chake, Pemba lakini wanafanya mazoezi ya siri sana kujiandaa na mtanange huo katika Uwanja wa Gombani, ambako wamekuwa wakiwafukuza waandishi wa habari waliokuwa wakifuatilia jinsi wanavyojifua.

Hii si mara ya kwanza kwa Yanga kujichimbia mafichoni kwenye hoteli hiyo, kwani huko ndiko walikopata dawa ya kuwachapa mahasimu wao mabao 2-0 katika mzunguko wa kwanza.

Mbali na kambi hiyo ambayo inawapa uhakika wa ushindi Wanajangwani hao, habari za uhakika ambazo MTANZANIA limezipata kutoka visiwani Pemba zinaeleza kuwa afya za wachezaji nyota wa timu hiyo waliokuwa majeruhi zimeimarika.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na beki, Haji Mwinyi, wameimarika na tayari wameanza kufanya mazoezi ya pamoja na wenzao tayari kwa kuivaa Simba keshokutwa.

“Cannavaro na Mwinyi ambao walikosa mechi zilizopita za Ligi Kuu lazima watacheza dhidi ya Simba baada ya afya zao kuimarika na kurejea katika viwango vyao, hivyo hatuna wasiwasi na mchezo wa keshokutwa,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kilitamba kuwa Yanga wamepania kuifanyia Simba ‘surprise’ ambayo haijawahi kutokea, hivyo wapenzi na mashabiki wajiandae kwa mambo mazuri waliyoyaandaa kutoka Pemba.

Yanga wanaoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kwa kujikusanyia pointi 43 nyuma ya vinara Simba, wamepania kuwafunga wapinzani wao na kurejea kileleni kwa kishindo huku wakitaka kuendeleza heshima ya kuwafunga mahasimu wao katika msimu huu wa ligi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles