Na Asifiwe George, Dar es Salaam
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama, limejipanga kuhakikisha mchezo wa Simba na Yanga utakaochezwa Februari 20 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa unachezwa katika hali ya amani na usalama.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, alisema mashabiki wa timu hizo hawataruhusiwa kuingia uwanjani na chupa za maji, silaha ya aina yoyote na hawatoruhusiwa kupaki magari ndani ya uwanja isipokuwa maeneo maalumu tu.
Kamanda Sirro alisema barabara zote zinazoingia katika uwanja huo zitafungwa ili kupisha msongamano wa magari, pia kutakuwa na ukaguzi mkali katika milango yote mikubwa ili kuhakikisha wanaoingia uwanjani hapo hawana vitu vyenye uwezekano wa kuleta madhara kwa watazamaji.
“Ninawashauri wananchi kukata tiketi zao mapema kwenye vituo vilivyoainishwa na vyombo husika ili kuepuka usumbufu usiokuwa wa lazima na wale watakaolazimika kukata tiketi uwanjani hapo ninawashauri kufuata utaratibu uliopangwa.
“Kutakuwa na kamera za CCTV zitakazofungwa kuzunguka uwanja wote ili kusaidia kuimarisha ulinzi katika mechi hiyo, hivyo matukio yote muhimu yatarekodiwa,” alisema Kamanda Sirro.
Kamanda Sirro alisema kutakuwa na doria za mbwa wa polisi na farasi waliopata mafunzo ya kisasa ambao watazunguka nje ya uwanja kuimarisha ulinzi ili kuhakikisha mechi hiyo inamalizika kwa amani na utulivu.