JOHANES RESPICHIUS-DAR ES SALAAM
TANGU nchi ipate uhuru mwaka 1961, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeweza kupima viwanja milioni 1.36, mashamba 24,579 na vijiji 10,667.
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Upimaji na Ramani, Justo Lyamuya alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana.
Alisema mwaka wa fedha 2016/17 lipo lengo la kupima na kutoa hati 400,000 na kampuni zinazopima ardhi zinatakiwa kushirikiana na Serikali kuhakikisha lengo hilo linafanikiwa.
“Kwenye robo ya kwanza ya mwaka wa kuanzia Julai hadi Septemba 2016 umefanyika upimaji wa viwanja 32,303 na mashamba 76 ingawa upimaji mashamba umekuwa ukipungua huku viwanja vikiongezeka kutokana na maeneo mengi kugeuka kuwa ya mpango.
“Pia kuhusu upimaji wa ardhi ya maji, kwa kipindi cha miaka mitatu, Tanzania kwa kushirikiana na Jeshi la Maji la India imeweza kupima Bandari ya Dar es Salaam, Zanzibar na mkoani Pemba na kwa mwaka huu umefanyika upimaji wa bandari ya Tanga,” alisema Lyamuya.
Alisema tayari imekwisha kuandaliwa mikataba ya makubaliano na kuridhiwa kupima mipaka ya kimataifa yote ya bandarini na majirani.
Kuhusu maziwa makubaliano ya kweka mpaka ndani ya ziwa Tanganyika kati ya Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia na Burundi yameshafanywa na utekelezaji wake utaanza fedha zikipatikana.