22.2 C
Dar es Salaam
Sunday, June 16, 2024

Contact us: [email protected]

Wiki ya AZAKI 2024 yazinduliwa rasmi Dar

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation For Civil Society (FCS), Justice Rutenge, amesema katika kutekeleza Dira ya Taifa 2050 wananchi wanapaswa kupaza sauti zao kwa kutoa maoni  yatakayopelekea kupata Dira bora kwa maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Rutenge ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi rasmi wa Wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKI) 2024,  itakayofanyika Septemba 9 hadi 13 jijini Arusha ambapo zaidi ya washiriki 500 wanatarajiwa kushiriki.

Ameeleza kuwa maadhimisho hayo mwaka huu yamebebwa na kaulimbiu isemayo ‘Sauti, Maono na Thamani’ lengo likiwa ni kutoa fursa zaidi kwa wananchi kupaza sauti zao kwa pamoja ili kurahisisha mchakato mzima wa upatikanaji wa Dira hiyo.

“Kaulimbiu ya Wiki ya AZAKI mwaka huu, inalenga kuwa na Dira nzuri licha ya tofauti ya mitazamo ya watu na makundi, bado sauti zetu zinapaswa kuwa kitu kimoja ili kurahisisha mchakato wa Dira ya maendeleo ya Taifa 2050,” amesema Rutenge.

Aidha, amesema FCS inajukumu kubwa la kuziwezesha Asasi za Kiraia kushiriki kwenye maendeleo ya watu, na kwamba Wiki ya AZAKI itajumuisha Asasi mbalimbali zitakazoshiriki maadhimisho hayo.

Ameongeza kuwa, Wiki ya AZAKi  mwaka huu inafanyika mapema mwezi Septemba, tofauti na ilivyozoeleka ambapo hufanyika mwezi Oktoba tangu kuanzishwa kwake 2018, nakwamba lengo la mabadiliko hayo ni kuhamasisha wananchi kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Wiki ya AZAKI mwaka huu imefadhiliwa na Vodacom Foundation na wadau wengine wa maendeleo, zikiwemo Asasi za Kiraia, ambapo katika Wiki hiyo mambo mbalimbali yatajadiliwa ikiwemo njia zinazoweza kuleta thamani halisi na chanya kwa kufikia maono ya pamoja ya mustakabali wa nchi na kuimarisha ushirikiano baina ya Sekta Binafsi, Umma, na Asasi za kiraia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles