LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) limesema magonjwa ya mlipuko kama ebola na kipindupindu yanatarajiwa kuongezeka kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, uharibifu wa misitu na idadi kubwa ya watu kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO anayeshughulikia majanga ya dharura ya kiafya, Dk. Michael Ryan, alinukuliwa na Shirika la Habari la Uingereza (BBC) akisema magonjwa kama vile ebola yanatarajiwa kuwa maradhi ya kawaida katika maisha ya binadamu.
Kutokana na tahadhari hiyo, MTANZANIA ilimtafuta Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohammed Kambi, ambaye alisema wanalifahamu suala hilo hata kabla ya taarifa hiyo ya WHO kutokana na mazingira yalivyo kwa sasa, ikiwamo mabadiliko ya tabia nchi, ongezeko la watu na mwingiliano wa watu.
“Kwa vyovyote magonjwa hayo yataongezeka. Mambo yanayotakiwa kwa sasa na ambayo tayari yanafanyika kwanza ni jamii kujua hali hiyo na mara kwa mara tunatoa hizo taarifa.
“Pili iko mipango mingi tu na mikakati ya kushughulikia hayo mambo na tunalifanya hilo kwa kushirikiana wizara na sekta nyingine kwa sababu haya mambo yanahitaji sekta mbalimbali kwa pamoja kushirikiana.
“Lakini pia kuna mipango inahusisha nchi jirani, kwa mfano hivi ninavyozungumza niko Namanga (Arusha), hapa leo (jana) umefanyika ufunguzi wa zoezi la kuangalia utayari wa Kenya na Tanzania katika kudhibiti magonjwa ya mlipuko. Kwa hiyo yako mambo mengi yanafanyika kuhusu hilo suala,” alisema Profesa Kambi.
WHO imeonya kuwa juhudi zaidi zinahitajika katika kukabiliana na majanga ya kiafya kama vile ebola, kipindupindu na homa ya manjano.
Dk. Ryan alisema shirika hilo linaendelea kufuatilia kwa karibu visa 160 vya magonjwa kote duniani ambapo tisa kati yake vimetajwa kuwa katika kiwango cha tatu ambacho ni kiwango cha juu zaidi cha majanga ya dharura ya kiafya.
“Sidhani kama tumewahi kuwa katika hali kama hii ambapo tunashughulikia majanga mengi ya dharuru ya kiafya kwa wakati mmoja. Hii ni hali mpya ambayo imeanza kuwa ya kawaida, sioni visa hivi vikibadilika au kupungua,” alisema Dk. Ryan.
Taarifa ya WHO iliitaja Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuwa nchi inayokumbwa na mlipuko wa ebola zaidi.
Hadi sasa jumla ya visa 2,025 vya ugonjwa wa ebola na vifo 1,357 vimeripotiwa nchini DRC, huku juhudi za kukabiliana nao zikidaiwa kukwamisha na machafuko ya kisiasa yanayoendelea maeneo mbalimbali, hususan mashariki mwa nchi hiyo.
Inadaiwa kuwa kati ya Januari na Mei mwaka huu kulikuwa na jumla ya matukio 40 ya kushambuliwa kwa vituo vya afya.
Pia inadaiwa kuwa watu hawawaamini watoa huduma za afya, jambo linalosababisha watu wenye dalili za ugonjwa huo kukwepa kujitokeza kupata matibabu na kukwamisha juhudi za kuzuia kuenea kwa virusi vya ugonjwa huo.