25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

Mashirika ya umma yadaiwa mabilioni

NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

BAADHI ya taasisi na mashirika makubwa ya umma zimebainika kuwa vinara wa kutolipa kodi ya pango la ardhi huku nyingine zikidaiwa hadi Sh bilioni 40.

Hadi sasa Serikali inadai zaidi ya Sh bilioni 200 za kodi ya ardhi kutoka kwa taasisi na kampuni 207 za umma na binafsi.

Mashirika hayo yalibainika jana wakati wa mkutano baina ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, na wakuu wa taasisi, mashirika na kampuni zinazodaiwa kodi jijini Dodoma.

Akizungumza katika mkutano huo, Lukuvi alisema kumbukumbu walizonazo zinaonesha baadhi ya taasisi hizo hazijalipa kodi kwa miaka 10.

“Nimewaita kutokana na rekodi nilizonazo katika ofisi yangu, mnamiliki ardhi, lakini wengine mnadaiwa na wengine hamjawahi kulipa kabisa.

“Nawataka wadaiwa wote kulipa kodi zote na malimbikizo kufikia Juni 20 ili kukwepa aibu, fedheha na mkono wa sheria,” alisema Lukuvi.

Alisema zoezi la kuwafikisha wadaiwa sugu mahakamani litaanza Juni 21 ambalo litakwenda sambamba na kukamata na kuuza mali za wadaiwa husika.

“Nimeamrisha watu wangu wote wasione haya, awe ni masikini, mtumishi wa Serikali, tutafunga ofisi, tutakamata magari yenu ili mradi ulipe kodi.

“Ninyi UDSM (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) baada ya tarehe 20 tunaanzia pale Mlimani City, pale ndio patamu, wanapata fedha halafu hawalipi kodi.

“Kama bajeti haitoshi kwenye mikoa na wilaya ya huduma za maji mjue kuna watu wanawachelewesha, hawalipi kodi. Kila mmoja aseme hizi fedha analipa lini,” alisema.

Lukuvi alisema kuna baadhi ya wadaiwa wamemwandikia barua kuomba kufutiwa kodi na kusisitiza hakuna kodi itakayofutwa.

“Msingi wa shughuli na biashara zote mnazofanya ni ardhi, wengine wananiandikia barua wanaomba kufutiwa kodi, kwanini mnataka kufutiwa wakati ardhi ndio msingi wa biashara zenu?

“Ukiwa na kodi ya ardhi unatakiwa kulipa, kitakachorekebishwa ni zile takwimu zako sahihi, mimi sina mamlaka ya kufuta wala kupunguza hata shilingi,” alisema.

Alisema pia wanazo taarifa kutoka taasisi za umma ambazo zimekuwa zikitenga bajeti kwa ajili ya kodi ya ardhi, lakini hazilipi.

“Tunazo taarifa kwamba huwa mna bajeti, lakini kwa sababu taasisi nyingi za Serikali mmezoea kutolipa, mnaacha, lakini maji, umeme na vingine mnalipa,” alisema.

Alikishauri Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), wakati wa kukusanya kodi  ya ardhi zilipwe kwa wakati ili kuepuka taasisi husika kuja kulipa kwa adhabu.

Lukuvi alitolea mfano wa Kiwanda cha Dangote ambacho kililipa Sh milioni 800 Novemba 30 mwaka jana, lakini TIC ilihamisha fedha hizo Januari 30, kitendo kilichosababisha iongezwe adhabu ya Sh milioni 8.7.

“Nitachapisha makubaliano yenu baada ya tarehe 20, wananchi wengine wajipime wenyewe wanataka tuwafuate na polisi mlangoni au watalipa kwa hiyari.

“Ofisi za wilaya mwezi huu zinafanya kazi hadi Jumamosi, hivyo watu waende wakahakiki madeni yao na kulipa,” alisema Lukuvi.

Alisema pia awamu ya pili ya wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi itatangazwa hivi karibuni kwani tayari anayo orodha.

“Orodha ya pili ina watu 606 na wengine ni vigogo, sasa tusiaibishane, naiweka kwenye mitandao baada ya siku tatu,” alisema.

Katika mkutano huo, Lukuvi alisoma mtu mmoja mmoja na kiwango anachodaiwa huku akiwataka wenye vielelezo kama walishalipa wavioneshe.

MSAMAHA WA KODI

Alisema msamaha uliotolewa kuanzia Julai Mosi 2018 haukuhusu madeni na malimbikizo ya kodi yaliyokuwepo kabla ya mabadiliko ya sheria.

“Sheria haikusema kwamba ufutiwe na madeni ya nyuma, tutafanya tathmini tujue katika shughuli zako kama hakuna biashara na hapo ndipo msamaha utaupata… anayefikiri anastahili msamaha aandike barua,” alisema Lukuvi.

Pia alisema maeneo yote ya madini yaliyopewa leseni za uchimbaji lazima wachukue hati na waanze kulipa kodi.

TAASISI ZA UMMA

Baadhi ya taasisi za umma na viwango wanavyodaiwa ni TTCL Sh bilioni 40.1, Tanesco Sh bilioni 25.5, NARCO Sh bilioni 23.4, SUA Sh bilioni 10.7, TIC Sh bilioni 9.1, TAA Sh bilioni 8.1, Shirika la Elimu Kibaha Sh bilioni 5.5, Reli Asset Sh bilioni 4.1, Tanzania Sisal Board Sh bilioni 3.8, SIDO Sh bilioni 3.7 na NHC Sh bilioni 3.4.

Nyingine ni TRC Sh bilioni 2.8, UDSM Sh bilioni 2.3, TPA Sh bilioni 1.6, TBA Sh bilioni 1.5, NSSF Sh bilioni 1.6, NAFCO Sh bilioni 1.2, PSSSF Sh bilioni 1.2, MUST Sh bilioni 1.1, Bodi ya Sukari Sh milioni 878.9, Tantrade Sh milioni 737.4, TPDC Sh milioni 705.1, Chuo cha Ushirika Moshi Sh milioni 643.6 na Manispaa ya Moshi Sh milioni 635.

HATI ZA KIELEKTRONIKI

Lukuvi alisema tayari wameanza kutoa hati za ardhi kwa mfumo wa kielektroniki katika wilaya za Ubungo na Kinondoni na kuanzia Julai wataanza kuzitoa katika mkoa wote wa Dar es Salaam.

Alisema hadi sasa kuna hati 500 ziko tayari na kwa zile za mfumo wa zamani kwa Dar es Salaam ziko 7,000 ambazo zimeshalipiwa, lakini wahusika hawajaenda kuzichukua.

Waziri huyo alisema mwakani wataanza kupima ardhi yote nchini na kutoa hati za kielektroniki.

WADAIWA WAJITETEA

Katika mkutano huo, baadhi ya wadaiwa walionekana wakijaribu kujitetea na kutaka wapunguziwe kodi, lakini Lukuvi alisisitiza walipe kwanza madeni wanayodaiwa kisha watakaa kuzungumza kuhusu changamoto nyingine.

Mwakilishi wa SIDO alisema ana viwanja katika maeneo mbalimbali ya nchi, lakini kuna maeneo hana hati na kwamba alipoomba aliambiwa alipe deni kwanza.

“Ofa unayo? (Lukuvi alimuuliza mwakilishi SIDO)…ndiyo, hiyo ni kama hati unalipia kodi. Unavyoomba fedha za umeme, maji, simu uombe na za kulipia kodi ya ardhi,” alisema Lukuvi.

Mwakilishi kutoka Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), alisema kuna mawasiliano dhaifu kati ya taasisi na wizara na kusababisha badhi ya shughuli kutokwenda kwa haraka kama ulipaji wa kodi. 

Mshiriki mwingine alishauri kuanzia mwaka ujao wa fedha wapewe bili za viwanja vyote ili walipe kwa wakati mmoja na kupitia hundi moja tofauti na inavyofanyika sasa.

Lukuvi alimwagiza Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika wizara hiyo kushughulikia suala hilo kwa lengo la kupunguza gharama ya kuwafuata wateja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles