31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

WHO, UN wakosoa uamuzi wa Trump

GENEVA, USWISI

Mkurugenzi Mkuui wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus amekosoa hatua ya Rais wa Marekani, Donald Trump kusitisha ufadhili wa nchi yake kwenye shirika hilo, akisema si uamuzi sahihi kwa sasa.

Akizungumza muda mfupi baada ya Trump kutoa tangazo hilo jana, Ghebreyesus alisema kwa sasa WHO inaangalia zaidi hatua muhimu za kuokoa maisha ya watu dhii ya virusi vya corona na si vinginevyo.

“Hatuna muda wa kupoteza. Kwa sasa WHO inaangalia suala moja tu, kufanya kazi kuhakikisha inasaidia watu wote kuokoa maisha yao na kumaliza tatizo la Covid-19,” aliandika katika akaunti yake ya Twitter.

China ambayo pia Trump amekuwa akiitaja amba ilipendelewa zaidi ya WHO katika kuchukua hatua ya kupambana na janga hilo iliitaka Marekani kutekeleza jukumu lake kwa WHO baada ya Rais Trump kusitisha ufadhili katika shirika hilo, akikosoa jinsi  lilivyoshughulikia janga la virusi vya corona.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China, Zhao Lijian alisema kuwa janga la virusi vya corona limefika katika hatua ya kutisha na hivyo basi uamuzi wa Rais Trump wa kusitisha ufadhili kwa WHO utaathiri mataifa yote duniani.

Marekani ndio mfadhili mkubwa wa WHO, ikichangia zaidi ya Dola milioni 400 mwaka 2019 ambayo ni asilimia 15 ya bajeti ya shirika hilo la afya lenye makao yake Geneva.

Rais Trump ameishutumu WHO  kuficha ukweli kuhusu mlipuko wa virusi vya corona na badala yake kuamini kila taarifa iliyotolewa na China kuhusu virusi hivyo.

Hata hivyo, aliyekuwa mkuu wa idara ya ujasusi nchini Uingereza, John Sawers alisema itakuwa bora China kubebeshwa lawama badala ya WHO.

Sawers alisema kuwa anafahamu hasira aliyo nayo Marekani kutokana na taarifa walizokuwa wamezificha kuhusu virusi vya corona.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Ryabkov pia aliitaka Marekani kukomesha mashambulizi na hatua zake za uhasama dhidi ya WHO.

Ryabkov, alisema kuwa WHO linafungamana kikamilifu na hati yake na linaheshimiwa na aghlabu ya nchi za dunia wakiwemo wasomi na madaktari wabobezi. Aliitaka Marekani kuwajibika kuhusiana na shirika hilo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas aliukosoa uamuzi wa Rais Trump akisema kuwa kinachohitajika sasa ni kuliimarisha shirika la afya duniani.

Kupitia ukurusa wake wa Twitter, Maas ameandika: “Lawama hazisaidii. Virusi vya Corona havijui mipaka. Tunahitajika kushirikiana katika vita hivi dhidi ya Covid-19 hasa kuimarisha shirika la WHO”.

Huku hayo yakiarifiwa, Ofisi ya Kansela Angela Merkel imependekeza kwa majimbo yote 16 ya nchi kuendelea na utekelezwaji la agizo la watu kutokaribiana hadi Mei 3 ili kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Kuhusu maambukizi ya corona Ujerumani, Lothar Wieler ambaye ni mkuu wa taasisi ya utafiti ya Robert Koch alisema: “Kwa sasa tuna uwezo wa kutosha katika hospitali zetu, hasa vitanda katika chumba cha wagonjwa mahututi na vifaa ya kusaidia wagonjwa kupumua.”

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres alisema kuwa huu si wakati mzuri wa kupunguza ufadhili WHO.

Kupitia taarifa, Guterres alisema kuwa sio tu WHO bali mashirika yote ya kibinadamu yanayopambana na janga la virusi vya corona hayafai kupunguziwa ufadhili hasa wakati huu.

Guterres ametoa wito wa mshikamano baina ya jamii ya kimataifa katika vita dhidi ya janga la virusi la Corona.

Akitangaza kusitisha ufadhili wake kwa WHO, Rais Trump alisema, kwa muda mfupi atasimamisha mchango wa Marekani kwa shirika hilo huku ikifanywa tathmini ya jinsi shirika hilo lilivyoshughulikia mlipuko wa virusi vya corona mara tu baada ya kuzuka. 

Trump alidai katika mkutano na Waandishi Habari katika Ikulu ya White House kwamba iwapo WHO lingefanya kazi yake vizuri na kutuma wataalamu wa afya China, basi mlipuko huo ungeweza kudhibitiwa. 

Aliongeza kwamba Shirika la WHO limeshindwa kutimiza jukumu lake la msingi na lazima liwajibishwe. 

Trump pia alisema shirika la WHO limeiunga mkono China kwa kutoa taarifa zisizo sahihi kuhusu virusi vya corona.

“Ninawapa muongozo utawala wangu kusitisha ufadhili wakati Shirika la afya duniani likiwa linachunguzwa katika majukumu yake yaliyoshindwa kuyatimiza katika kukabiliana na usambaaji wa virusi vya corona ,” Trump aliwaambia waandishi.

Marekani ndio mfadhili mkubwa wa WHO anayetoa ufadhili wa kiasi cha Dola milioni 400 ambayo ni asilimia 15 ya bajeti yake ya mwaka jana.

China ilichangia mwaka 2018-19 karibu Dola milioni 76 na yapata Dola milioni 10 katika ufadhili, kwa mujibu wa mtandao wa shirika la afya duniani.

Shirika hilo lilitenga kiasi cha Dola milioni 675 kukabiliana na magonjwa ya mlipuko na limeripotiwa kuwa litaongeza fedha hizo hadi karibu dola bilioni moja.

Marekani ina idadi kubwa ya maambukizi ya virusi vya corona duniani kwa kuwa na wagonjwa 608,377 na vifo vilivyotokana na ugonjwa huo kufikia 25,981.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles