26.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 30, 2024

Contact us: [email protected]

WHC KUJENGA NYUMBA 36 ZA POLISI, WALIMU KANDA YA ZIWA

Na JUDITH NYANGE-MWANZA


KAMPUNI ya Ujenzi wa Nyumba za Watumishi (WHC), inatarajia kujenga nyumba 36 za makazi kwa ajili ya walimu na polisi mkoani Mwanza, Simiyu na Geita ili kupunguza adha kwa watumishi  wanaoishi kwenye mazingira magumu kwa mikoa hiyo.

Akizungumza na MTANZANIA juzi,  Ofisa Mtendaji Mkuu wa WHC, Dk. Fred Msemwa, alisema  mradi wa nyumba za walimu unatarajia  kuanza kutekelezwa Mei mwaka huu na katika wilaya za Ukerewe, Magu, Busega na  Mbogwe huku ule wa makazi ya polisi ukitekelezwa kwenye Wilaya ya  Nyang'wale.

Alisema lengo la mradi huo ni kutatua tatizo la makazi kwa watumishi wanaofanya kazi na kuishi katika mazingira magumu hasa wale wanaolazimika kuishi kwenye maeneo yao ya kazi.

“Mradi utahusisha ujenzi wa nyumba  sita za walimu zenye vyumba viwili vya kulala, choo, sebule na jiko kila shule katika sekondari za Nduruma wilayani Ukerewe na Shishane iliyopo Magu mkoani Mwanza, Nyaruhanda (Busega-Simiyu) na Mbogwe (Mbogwe-Geita) na utagharimu Sh milioni 700.

“Pia tutajenga nyumba 12 za askari polisi waliopo katika Wilaya ya  Nyang'wale mkoani Geita ambao tumeona wanafanya kazi katika mazingira magumu sana na mradi huo  utagharimu Sh milioni 400.

“Miradi hiyo ni endelevu na wilaya ambazo hazikufikiwa katika awamu hii ya kwanza zitaendelea kufikiwa katika awamu nyingine kwa kuwa itatekelezwa  kwa mikoa yote ya Tanzania,” alisema Dk. Msemwa.

Aidha, Dk. Msemwa amewataka viongozi wa halmashauri zote ambazo miradi hiyo itatekelezwa kutoa ushirikiano wakati wa ujenzi ili kufanikisha lengo lililokusudiwa.

Miradi kama hiyo tayari imetekelezwa katika mkoa wa Mogogoro, Pwani, Mtwara, Dar es Salaam na Lindi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles