25.2 C
Dar es Salaam
Saturday, January 29, 2022

KITWANGA KUONDOA SHILINGI BAJETI YA MAJI

Na PETER FABIAN-MWANZA


MBUNGE wa Misungwi Mkoa wa Mwanza, Charles Kitwanga, amesema ataondoa shilingi katika bajeti ya Wizara ya Maji ili kuishinikiza kutekeleza ahadi ya Rais Dk. John Magufuli ya kuupatia maji ya Ziwa Victoria mji wa Misungwi.

Akizungumza na wananchi kutoka Kata za Fela, Koromije na Lubili wilayani humo, Kitwanga alisema amesikiliza kero za wananchi na kuwaomba wawe na uvumilivu wakati anajiandaa kuwasilisha hoja mbili binafsi ya njaa na maji kwenye kikao cha Bunge la Bajeti kinachoendelea Mjini Dodoma.

“Hii kero ya majisafi nimeisikia na imenigusa, inaninyima usingizi kutokana na jiografia ya Jimbo na Wilaya ya Misungwi kuwa na baadhi ya maeneo yenye ukame kila mara inafikirisha, lakini hili la kukosa maji kiasi cha wananchi kuhangaika na kuchangia maji na mifugo katika malambo linaumiza zaidi.

“Lakini kwa hili ninaenda kuondoa shilingi kwenye bajeti ya Wizara ya Maji hadi wanipe uhakika wa maji katika wilaya hii, katika kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita, Rais Magufuli aliwaahidi wananchi kwamba suala la maji wasinisumbue akasema akichaguliwa kuwa rais maji yatafika Misungwi,” alisema.

Alisema anakwenda bungeni na atakumbushia suala hilo ambapo asipopata majibu ya kuridhisha kuhusu kadhia wanayopata wananchi wake ataondoa shilingi katika bajeti hiyo.

Mbunge huyo pia alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Misungwi, Eliud Mwaiteleke, kushirikiana na wataalamu wake kupita vijiji vyote na kufanya tathmini upya ikiwamo kuvikagua visima vya majisafi ili kuona kama vinatoa maji na kama havitoi ili waweze kuanza mkakati wa kuvitengeneza ikiwa ni pamoja na kutafuta wafadhili wa kusaidia kupata visima vingine kusaidia kupunguza kero hiyo.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
177,207FollowersFollow
532,000SubscribersSubscribe

Latest Articles