Na Kulwa Mzee -DAR ES SALAAM
WAFANYABIASHARA wawili walioingiza magari matatu ya kifahari kwa kuyaficha katika kontena wakidai limebeba nguo za mtumba, wametiwa hatiani na watafilisiwa magari yote na kutakiwa kulipa fidia ya jumla ya Sh milioni 100.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha baada ya washtakiwa kukiri makosa mawili yaliyokuwa yakiwakabili.
Washtakiwa Sultani Ibrahimu (36) raia wa Uganda na Ramadhani Hamis (48) maarufu Ukwaju, wanadaiwa kutumia nyaraka za uongo Januari 18, mwaka huu Makao Makuu ya Bandari, Dar es Salaam, kwamba walibeba mitumba katika kontena wakati walibeba magari ya kifahari matatu na shtaka la pili kusababisha hasara ya zaidi ya Sh milioni 190.
Akitoa hukumu, Hakimu Mkeha alisema: “Nimezingatia hoja zilizowasilishwa na pande zote mbili, mahakama inaamuru magari yafilisiwe, lakini si kwa matakwa ya washtakiwa, bali sheria inatamka hivyo.”
Alisema thamani ya magari hayo ni kubwa, Sh 287,779,536 ambayo ni kubwa kuliko hasara inayodaiwa kusababishwa.
“Kutokana na hoja hizo, kwa kosa la kwanza kila mshtakiwa anatakiwa kulipa faini ya Dola za Marekani 10,000 akishindwa atakwenda jela miaka mitatu na kosa la pili kila mshtakiwa anatakiwa kulipa faini ya Sh milioni tano, akishindwa atakwenda jela miaka mitatu,” alisema.
Awali baada ya kukiri makosa hayo, washtakiwa walisomewa maelezo ya awali kwamba kati ya Desemba mosi 2016 na Machi 2017, pamoja na watu wengine wanaoishi Uingereza, walikubaliana kuingiza magari Tanzania.
Inadaiwa Oktoba 13, 2016 kupitia nyaraka ya kuingizia mizigo bandarini namba 5709947971, washtakiwa na wenzao walioko Ulaya walisafirisha kontena namba MRKU 3049836 ambalo lilibeba magari matatu ya kifahari aina ya Range Rover Evoc yenye chesesi namba Salva, 2AE9DH766530, Range Rover Sports yenye chesesi namba Salga 2JE6A1596651 nyeusi na gari la tatu aina ya Audio Q3 yenye chesesi namba WAUZZZ844 DRO28763 ya rangi ya kijivu.
Inadaiwa katika Makao Makuu ya Bandari, Dar es Salaam walitoa tamko la uongo kwamba kontena hilo lina mitumba ya nguo, viatu na magodoro kwa lengo la kukwepa kodi huku wakijua kwamba thamani ya mali waliyotamka ni ndogo ukilinganisha na magari waliyobeba.
Kutokana na tamko hilo la uongo, walisababisha maofisa forodha wa Mamlaka ya Mapto kukadiria kodi ya chini ya Sh 31,548424 badala ya kodi sahihi waliyopaswa kulipa Sh 190,923,267.76 .
Wakili wa Serikali Mkuu, Mutalemwa Kishenyi, alipotakiwa kusema lolote kuhusu washtakiwa kabla ya mahakama kutoa adhabu, alisema ni wakosaji wa mara ya kwanza, aliiomba mahakama ikitoa adhabu katika kosa la pili itoe amri ya faini, fidia na magari yataifishwe.