23.4 C
Dar es Salaam
Friday, June 21, 2024

Contact us: [email protected]

MBUNGE CHADEMA ASHINDA RUFAA YA UBUNGE

Na MURUGWA THOMAS -TABORA

MAHAKAMA ya Rufaa imetupilia mbali rufaa iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge wa Buyungu, Christopher Chizza (CCM) dhidi ya Mwalimu Kasuku Bilago (Chadema) kupinga matokeo ya uchaguzi.

Uamuzi huo ulitolewa jana katika kikao cha mahakama hiyo kinachoendelea mkoani Tabora.

Jopo la majaji wa mahakama hiyo chini ya Uenyekiti wa Jaji Benard Luanda akisaidiwa na Jaji Bathuel Mmilla na Jaji Rehema Mkuye, walitupilia mbali rufaa hiyo kutokana na kutokidhi matakwa ya sheria.

Wakili wa mjibu rufaa, Tundu Lissu, akiongea nje ya mahakama, alisema mahakama hiyo imejiridhisha na kuamua kutoendelea kusikiliza shauri hilo baada ya kugundua kwamba rufaa hiyo haikidhi matakwa ya kisheria.

“Kukosekana kwa ‘drawer oder’ ndiko kulikosababisha kutupiliwa mbali kwa rufaa ya Chizza,” alisema Lissu.

Lissu alisema kuwa kwenye kesi kubwa kama hiyo ambayo ina masilahi kwa umma, mahakama zinatakiwa zisifungwe na kanuni zake.

Alisema mahakama inatakiwa izingatie ibara ya 107 (b) 2 (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoitaka itende haki bila ya kufungwa na kanuni.

Rufaa hiyo inatokana na uamuzi wa Mahakama Kuu iliyoendesha kikao chake Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, baada ya kuyatupa madai yaliyowasilishwa na Chizza ya kupinga matokeo yaliyompa ushindi mbunge wa sasa.

Awali katika shauri hilo namba 194/2016 lililosikilizwa na Jaji Paul Kiwelo, alitupilia mbali malalamiko yote yaliyowasilishwa na Chizza ambaye alizidiwa kwa kura 57 na mpinzani wake.

Hiyo inakuwa ni rufaa ya pili kwa Chadema kushinda baada ya ile ya kwanza ya Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya iliyofunguliwa na mpinzani wake Steven Wasira.

Mahakama hiyo ya Rufaa inatarajiwa kuamua hatima ya ubunge wa Mbunge wa Longido, Onesmo ole Nangole (Chadema) ambaye alivuliwa ubunge Juni 29, mwaka jana na  Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles