26.7 C
Dar es Salaam
Saturday, February 24, 2024

Contact us: [email protected]

TAHARIRI: HEKO TANESCO KWA MABADILIKO CHANYA

MOJA kati ya habari zilizomo katika gazeti hili, ni hatua ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kufanikiwa kukusanya Sh bilioni 41 kutokana na madeni waliyokuwa wakidai.

Meneja Mwandamizi Hesabu wa Tanesco, Philidon Siyame, alisema hatua hiyo imetokana na mafanikio yaliyopatikana kutokana na utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli.

Alisema wakati Rais Magufuli anaingia madarakani kulikuwa na deni la Sh  bilioni 275.

Kwamba katika fedha hizo, Shirika la Umeme Zanzibar ( ZECO), lilikuwa linadaiwa Sh bilioni 180 na taasisi binafsi Sh bilioni 95.

Lakini baada ya kampeni ya kata iliyotangazwa na Rais Magufuli, wamefanikiwa kukusanya Sh bilioni 41 ambazo zimetokana na ZECO kulipa Sh bilioni 18, taasisi nyingine za Serikali Sh bilioni 18 na taasisi binafsi Sh bilioni 5.

Hii ni hatua ya kupongezwa kutokana na ukweli kuwa, kabla ya agizo la Rais Magufuli shirika hilo halikuwa na ujasiri wa kukusanya madeni yake kutokana na sababu mbalimbali ambazo wakati mwingine zilichangiwa na kelele au maamuzi ya kisiasa jambo ambalo huwafanya maofisa wake kushindwa kuchukua hatua kwa hofu ya kuwajibishwa.

Lakini sasa kutokana na kauli na misimamo thabiti ya Rais Magufuli la kulitaka shirika hilo kukata umeme kwa taasisi, idara, wizara na hata sekta binafsi kutokana na madeni, limefanikiwa kukusanya kiasi hicho kikubwa cha fedha.

Kwamba kabla ya Rais Magufuli kutangaza kampeni ya ‘KA-TA’, Tanesco walikuwa na uwezo wa kukusanya mapato ya shirika kwa asilimia 90 kwa mwezi, lakini kwa sasa wamevuka malengo na kufikia makusanyo ya asilimia 104 ya deni lote la wadaiwa sugu.

Mbali na hayo, ni wazi yapo pia mafanikio kadhaa katika uanzishwaji na uendelezwaji wa miradi ya mikakati kama vile mradi mkubwa wa kufua umeme wa gesi asilia wa Kinyerezi II utakaozalisha Megawati 240.

Inaelezwa kuwa awamu ya kwanza ya mradi huo utakamilika Desemba mwaka huu ambapo umeme huo utaingizwa kwenye gridi ya taifa sambamba na upanuzi wa mradi wa Kinyerezi I wenye ambao una uwezo wa kuzalisha Megawati 185 za umeme.

Licha ya hali hiyo pia kuna mradi wa usafirishaji wa umeme  North East Grid utakaoanzia Dar es Salaam, Chalinze hadi Arusha wa msongo wa Kilovolti 400 pamoja na mradi wa usafirishaji umeme Kilovolti 220 kutoka Makambako hadi Songea.

Kwa hatua hii sisi MTANZANIA tunapongeza mafanikio haya makubwa yaliyofanywa na Tanesco chini ya menejimenti yake kupitia Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Dk. Tito Mwinuka.

Kwa hakika inawezekana Tanesco wakapiga hatua na kufikia ndoto ya kuwa na umeme wa uhakika sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya umeme iliyochakaa na kuweka mipya ambayo itakuwa mkombozi kwa Watanzania wote.

Sisi MTANZANIA tunaamini nchi yetu inaweza kupiga hatua na kufikia uchumi wa kati ambao unachangizwa na ujenzi wa viwanda vitakavyozalisha kwa kutegemea nishati ya umeme.

Hivyo ni wakati wa Tanesco kuendeleza mafanikio waliyofikia sasa ili kuhakikisha azma ya Rais Magufuli ya kuwa na Tanzania ya viwanda inafikiwa, ikizingatiwa umeme ni nyenzo muhimu katika utekelezaji wa hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles