Na CLARA MATIMO- MWANZA
WAKAZI wa Kata ya Kayenze Wilaya ya Ilemela wameiomba Serikali kufanya maboresho katika sekta ya afya ili huduma zinazotolewa kuanzia zahanati hadi hospitali za rufaa za mikoa na taifa zizingatie mahitaji ya watu wenye ulemavu.
Ombi hilo lilitolewa jijini hivi karibuni kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Chama cha Watu Wenye Ulemavu Tanzania (CHAWATA) Wilaya ya Ilemela ambao ulilenga kuwaelimisha jamii kuhusu haki za watu wenye ulemavu.
Walisema watu wenye ulemavu hupata changamoto mbalimbali wanapokwenda kupata huduma za afya kutokana na maeneo mengi yanayohudumia jamii mbalimbali kutozingatia mahitaji ya makundi maalum.
“Ukienda kwenye hospitali za serikali hakuna hata wataalamu wa afya ambao wanaelewa lugha za alama wakati inatakiwa wawepo kwa sababu nchi yetu ilikwisha kusaini mkataba wa kimataifa wa watu wenye ulemavu.
“Hivyo ni lazima kila jambo la maendeleo linalofanywa lizingatie mahitaji maalum yanayowahusu watu hao.
“Pia nchi yetu ina sera ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2009 na sheria yake ya mwaka 2010 lengo la yote haya ni kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu zinalindwa.
“Sasa kama tutawanyanyapaa kuanzia kwenye huduma za umma na jamii ambazo ni muhimu kwa maisha ya kila siku nani atawasaidia?” alihoji Belita Misalaba.
Mwenyekiti wa Chawata Kata ya Kayenze, Ally Salum, aliwataka madereva kuwa makini wanapoendesha vyombo vya moto kuepuka kuongeza idadi ya watu wenye ulemavu katika jamii.
Mwezeshaji wa mkutano huo kutoka Chawata Ilemela, Adam Ndokeji, alisema ni wajibu wa jamii kuwalinda watu wenye ulemavu kwa kuhakikisha miundombinu ya barabara, vyoo, shule na ofisi za serikali zinajengwa kwa kuzingatia mahitaji ya watu hao.