24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MANISPAA YA UBUNGO YAJITOSA KULIPA FIDIA GOBA

Na JONAS MUSHI-DAR ES SALAAM


meya-wa-manispaa-ya-ubungo-boniface-jacob

MEYA wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob amesema manispaa hiyo italipa fidia kwa watu watakaoachia maeneo ya huduma za jamii  kupisha mradi wa upimaji, upangaji na urasimishaji wa maeneo ya makazi.

Mradi hiyo  unatekelezwa na Kampuni ya Upimaji na Upangaji Makazi (HUSEA) katika Mtaa wa Kunguru Kata ya Goba,  Dar ea Salaam.

Alikuwa akizungumza na wananchi kwenye mkutano ulohusisha wakazi wa mtaa huo na  Kampuni ya HUSEA.

Kampuni hiyo ilikuwa   ikiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo ambao umefikia hatua ya upimaji baada ya kukamilisha upitiaji wa mipaka.

“Ili miradi ya urasimishaji makazi iweze kufanyika vizuri bila   usumbufu ni lazima halmashauri tusaidie kulipa fidia  itakapoonekana kuna uhitaji wa maeneo ya huduma za jamii kama shule, zahanati, viwanja vya michezo na barabara ili upangaji ufanyike kisasa,” alisema Jacob.

Hata hivyo, alisema fidia haitalipwa kwa watu ambao wanatakiwa kupisha upanuzi wa barabara kwa kusogeza hatua chache na badala yake watalipwa wale ambao barabara italazimika kukatiza kwenye viwanja vyao kwa mujibu wa wataalamu wa upangaji.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mradi huo, Mwenyekiti wa HUSEA, Renny Chiwa, alisema mtaa huo una uhaba wa maeneo ya huduma za jamii yatakayoendana na wingi wa watu waliopo.

“Katika hatua za awali za kupitia mipaka tumeona kuna changamoto ya uhaba wa maeneo ya kutosha ya huduma za jamii huku baadhi ya maeneo yakiwa hayapitiki kutokana na kukosekana   barabara,” alisema Chiwa.

Alisema mradi huo ni shirikishi yamekuwa yakifanyika mazungumzo na baadhi ya watu ambao viwanja vyao vinazuia barabara na kuingilia maeneo ya wazi waweze kuachia kwa ridhaa yao.

Mkurugenzi wa Upangaji wa Vijiji na Miji kutoka Wizara ya Ardhi na Makazi, John Lupala, alisema ili kufanikisha mradi huo kwa haraka  atapangwa Ofisa Ufuatiliaji kutoka wizarani ashirikiane na HUSEA katika mradi huo wa Mtaa wa Kunguru.

“Kama mtaenda kwa umoja huu itakuwa rahisi kwa Kamishna wa Ardhi kuja kutolea hati hapa mtaani kwenu  kuondoa usumbufu wa kwenda wizarani kufuatilia hati zenu,” alisema Lupala.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles