30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

TUTARAJIE HAYA MZUNGUKO WA PILI VPL

ZAINA IDDY NA MARTIN MAZUGWA


kichuya

HIVI sasa wadau wa soka nchini wanahesabu siku kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2016/17, Desemba 17, mwaka huu, kwa michezo minne kurindima katika viwanja tofauti.

Timu hizo pamoja na bingwa mtetezi, Yanga, zitacheza mechi 15 za lala salama ili kukamilisha idadi ya michezo 30 ya mzunguko mzima wa ligi msimu huu, baada ya awali kushuka dimbani mara 15.

Yapo mengi yaliyojiri katika michezo 15 ya awali msimu huu, ikiwemo vurugu viwanjani, uharibifu wa miundombinu, malalamiko ya waamuzi na kushushiwa kipigo, ushindani wa timu pamoja na ule wa mchezaji mmoja mmoja na mengineyo.

Katika kuelekea mzunguko wa lala salama, pia yapo ya kuyatarajia kulingana na mfumo wa soka letu la bongo na SPOTIKIKI leo inakuletea baadhi ya mambo ambayo tutarajie kuyaona.

Makocha wapya kwenye timu

Kila timu imeonekana kujiimarisha kulingana na mahitaji yake, wakati zipo baadhi zikisajili wanandinga wapya, lakini pia zipo zilizobadili mabenchi yao ya ufundi, katika timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo, hadi sasa ni timu sita pekee zilizofanya maamuzi ya kubomoa mabenchi yao ya ufundi, wakiwamo Yanga, ambao wamewaleta Wazambia wawili; Kocha Mkuu George Lwandamina aliyekuwa akiinoa Zesco United ambaye amevaa viatu vya Hans van der Pluijm aliyepewa majukumu mapya ya Ukurugenzi wa Ufundi na  mwingine, Noel Mwandila, aliyepewa kazi ya ukocha wa viungo.

Kwa upande wa Maafande wa JKT Ruvu, wao wameamua kuachana na kocha wao, Malale Hamsini na kumpa ulaji Bakari Shime, aliyekuwa akikinoa kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, huku Malale akiula kwa Ruvu Shooting.

Mwadui wao baada ya kuondokewa kwa kocha wao, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, wameamua kumpa viatu vyake Ally Bushiri, aliyewahi kukinoa kikosi cha Zanzibar Heroes, wakati Maafande wa Tanzania Prisons wakimkabidhi kijiti cha ukocha Abdallah Juma, kutokana na kuvunja mkataba na Meja mstaafu Abdul Mingange.

Sura mpya

Katika kipindi cha dirisha dogo la usajili mara nyingi si timu zote zinazofanya usajili na hivyo ndivyo ilivyokuwa msimu huu katika usajili uliofunguliwa Novemba 15, ambao unatarajiwa kufungwa Desemba 15, mwaka huu.

Hadi sasa baadhi ya timu zimeshafanya usajili, ambapo Yanga wamemuongeza kiungo mkabaji Justine Zulu kutoka Zesco ya Zambia, huku wakitajwa kuachana na Mbuyu Twite, Simba wao wamemsajili kipa Mghana Daniel Agyei, akitajwa kuchukua nafasi ya Mcongo Mussa Ndusha, ambaye amekitumikia kikosi cha Wekundu wa Msimbazi michezo miwili tangu alipojiunga nayo akitokea DC Motema Pembe, Azam wakiwasajili wanandinga watatu ambao ni mzawa Joseph Mahundi na Waghana Yahaya Mohammed na Samuel Afful.

Mbeya City wao licha ya kutotangaza rasmi, lakini wameshasajili wanandinga Hood Mayanja, Majaliwa Mbaga, Titto Okello, wakati Kagera ikinasa saini ya kipa Juma Kaseja na Mohamed Faki, huku Majimaji wakimnasa Kelvin Sabato na Wazir Salumu.

Vita ya ubingwa na kushuka daraja

Katika michezo 15 ya mzunguko wa kwanza, Simba ndio walimaliza wakiwa kileleni, baada ya kukusanya pointi 35, wakipishana pointi mbili na watani zao wa jadi, Yanga, wenye alama 33, wakishika nafasi ya pili, huku Azam FC wao wakiwa namba tatu kutokana na kuwa na pointi 25 kibindoni, wakati Kagera Sugar  akiwa na alama 24, Mtibwa Sugar wakikamilisha tano bora katika msimamo huo, baada ya kujizolea pointi 23.

Katika msimamo huo, ni wazi vita ya ubingwa inawahusu zaidi Simba na Yanga, zinazopishana kwa pointi mbili, lakini pia upo uwezekano wa Azam kuingia katika kinyang’anyiro hicho, licha ya kupishana pointi 10 na anayeongoza ligi hiyo, wakati huo huo Kagera Sugar na ndugu zao Mtibwa wao wakipigania kubaki katika tano bora.

Wakati vita ya kuwania ubingwa ikizihusu timu tatu za juu, kwa upande wa zinazoburuza mkiani kunawezekana kukawa na ushindani mkubwa kutokana na idadi ndogo ya pointi wanazopishana, lakini pia kila mmoja akihitaji kusalia kwenye ligi hiyo msimu unaokuja.

Katika msimamo huo, Toto Afrika ndiye anayeburuza mkia akiwa na pointi 12 , akifuatwa na Mwadui wenye alama 13 nafasi ya 15 , wakati nafasi ya 14 ikishikwa na JKT Ruvu, wenye pointi sawa na Mwadui, lakini wakipishana kwa idadi ya mabao ya kufungwa na kufunga, huku anayekamilisha nafasi tano za chini ni Majimaji na Mbao FC wenye alama 16 kila mmoja.

Bingwa kabla ya ligi kufika kikomo

Katika msimu uliopita wa ligi ilishuhudiwa Yanga, aliyekuwa bingwa akitangaza ubingwa wake jijini Mbeya, alipokuwa akimenyana na Mbeya City, zikiwa  zimesalia mechi mbili kabla ya ligi kufika tamati, huku akiwaacha wapinzani wao wa jadi, Simba kwa alama 11,  na wao kuwa na pointi 73, wakifuatwa na makamu bingwa, Azam waliofikisha pointi 64.

Hali hiyo inaweza kujirudia tena msimu huu, licha ya kuwa hadi sasa, timu shindani kwenye kinyang’anyiro cha ubingwa (Simba na Yanga) kupishana kwa pointi mbili pekee katika msimamo, jambo ambalo litachangia ushindani mkubwa kwenye michezo yao ya mzunguko wa pili ili kuweza kutimiza lengo la kutwaa ndoo.

Vurugu viwanjani

Suala la vurugu viwanjani ni jambo la kawaida na ambalo linatarajiwa kutokea, hususan zinapocheza timu zenye upinzani katika soka, kwani si mara moja tumeshuhudia vitu vikiharibiwa katika viwanja mbalimbali kipindi mashabiki wanaposhindwa kukubaliana na matokeo yaliyopatikana, huku wengine wakichukua sheria mkononi kwa kuwarushia chupa za maji waamuzi na wachezaji.

Mfano mzuri ni katika mzunguko wa kwanza msimu huu pale zilipokutana timu za Simba na Yanga, Oktoba Mosi dimba la Taifa, mechi iliyochezeshwa na mwamuzi Martin Saanya kutoka Morogoro.

Katika mchezo huo, vurugu zilianza kabla ya mchezo, baada ya mashabiki kutaka kuingia uwanjani kwa nguvu, licha ya wanausalama kuwazuia kutokana na idadi kubwa ya walioingia, jambo lililosababisha kuvunjwa kwa mageti ya uwanja na kurushwa kwa mabomu ya machozi, mbali na hilo, hali ilionekana kuwa mbaya zaidi, baada ya mshambuliaji wa Yanga, Amis Tambwe, kufunga bao lililokuwa na utata kabla ya Shiza Kichuya kuja kutuliza ghasia hizo kwa kusawazisha.

Kutokana na vurugu hizo timu za Simba na Yanga zililazimika kulipa gharama za uharibifu na kuzuiwa kutumia uwanja  huo, kiuhalisia ni vigumu kudhibiti vurugu za mashabiki viwanjani, lakini bado viongozi wanaweza kuliwekea mikakati bora itakayopunguza jambo hilo  ambalo hugharimu maisha ya watu.

Kitendawili cha mfungaji bora

Katika kuwania kiatu cha ufugaji bora msimu huu, hali inaonekana ni tofauti na uliopita, kutokana na mzawa Shiza Kichuya wa Simba kujitokeza kupambana na wageni.

Katika msimamo wa ufungaji, Kichuya anaongoza kwa kufunga mabao tisa, akifuatiwa na mfungaji bora aliyepita, Amis Tambwe wa Yanga mwenye mabao saba sawa na Rashid Mandawa (Mtibwa Sugar) na Simon Msuva (Yanga), wakati John Bocco kutoka Azam akiwa amecheka na nyavu mara sita.

Hali hii ni tofauti na msimu uliopita, ulioonekana kutawaliwa na wageni, kwani Tambwe alichukua kiatu hicho akiwa na mbao 21, akifuatiwa na Hamis Kiiza wa Simba mabao 19 na Donald Ngoma aliyezichungulia nyavu za wapinzani mara 17, wote wakiwa wanandinga wa kigeni.

Panga pangua ya ratiba

Ingawa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetoa   ratiba ya ligi mzunguko wa pili na kujinasibu kutumia weledi mkubwa utakaozuia suala la panga pangua ya ratiba hiyo, lakini ukweli utabaki kuwa jambo hilo halitaepukika mzunguko huu wa lala salama.

Hii inatokana na mashindano ya kimataifa, ambapo timu za Yanga na Azam zitakuwa zikiiwakilisha nchi  na kila watakavyofanikiwa kupiga hatua moja mbele, ndivyo itakavyolazimika ratiba zao za ligi ya nyumbani kusogezwa mbele.

Yanga ina kibarua kigumu cha kushiriki michuano ya Klabu bingwa Afrika  mwakani, ambayo mwaka huu iliishia hatua ya awali, kabla ya kuja kuondolewa pia Kombe la Shirikisho kwenye hatua ya makundi, wakati Azam wao wanaiwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho waliyotolewa hatua ya pili ya michuano hiyo mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles