HADIA KHAMIS NA REHEMA ABDALLAH (A3), DAR ES SALAAM
WAGONJWA wenye matatizo ya mfumo wa njia ya haja ndogo ambao hujulikana kitaalamu kama ‘Urolojia’ wameongezeka kwa kasi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Kutokana na ongezeko hilo, uongozi wa hospitali hiyo umeanzisha idara maalumu inayoshughulikia matatizo hayo.
Mkurugenzi wa Idara ya Urolojia, Dk. Ryuba Nyansogoro, alisema wagonjwa wanaofika katika kliniki hiyo ni wengi ukilinganisha na idara nyingine.
Alisema kwa wiki moja wanapokea wagonjwa 190, ambao kati yao 30 hufanyiwa upasuaji wa njia ya haja ndogo huku 120 wakifanyiwa upasuaji wa figo.
Dk. Nyansogoro alisema idara yake ina mpango wa kuanzisha vitengo vingine zaidi, vitakavyobobea kwenye upasuaji wa njia ya mkojo kwa kutumia hadubini (microscope).
Mbali na hilo, wataanzisha kitengo cha watoto wenye matatizo ya mkojo pamoja na kutibu wagonjwa wenye saratani ya njia ya mkojo pamoja na wagonjwa wa fistula na makovu kwenye njia za mkojo.
Katika kuimarisha huduma hizo, Dk. Nyansogoro alisema wataendelea na utoaji wa huduma za upandikizaji wa figo kwa wagonjwa wenye matatizo hayo.
“Hata hivyo idara yetu inakabiliwa na uhaba wa wataalamu waliobobea kwenye fani hiyo pamoja na upungufu wa vyumba vya upasuaji, hivyo jitihada zaidi zinahitajika ili kuendana na mahitaji ya wagonjwa.