25.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yaonya wanaochezea sekta ya mkonge, yasisitiza uwekezaji mkubwa

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Ushirika na Umwagiliaji, Dk. Suleiman Serera, amesema Serikali haitamfumbia macho yeyote atakayechezea Sekta ya Mkonge kwa namna yoyote kwani sekta hiyo mtambuka ni ustawi wa maisha ya Watanzania wengi wa kaliba na kada tofauti.

Dk. Serera amesema hayo wilayani Korogwe mkoani Tanga wakati akizungumza na viongozi wa Vyama vya Ushirika na Masoko vya Mkonge (AMCOS) na kuongeza kuwa serikali inaendelea na mchakato wa kutatua changamoto ya upungufu wa mashine za kuchakata mkonge (korona) ambapo amewahakishia watapatiwa mapema kwani serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inafanya uwekezaji mkubwa katika eneo hilo la Sekta ya Mkonge.

“Ukizungumzia Mkonge Tanga ni maisha, ni siasa, ni kila kitu. Kwa hiyo mtu yeyote atakayecheza na Mkonge amecheza na siasa na maisha ya watu Tanga na sisi hatutaki tuharibikiwe.

“Ajenda ya 10/30 ni kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunaongeza pato la taifa la mazao mwaka 2030 kutoka asilimia nne ya sasa na mojawapo ya mazao ambayo yapo katika mpango huu ni Mkonge ambalo ni zao la maisha kwa ajili ya wakazi wa Tanga na maeneo mengine nchini,” amesema.

Pamoja na mambo mengine, amezipongeza AMCOS hizo tano za Magunga, Magoma, Hale, Kibaranga na Ngombezi kwa kuwa na ushirika imara ambapo amesema hatua hiyo itawasaidia kuhakikisha ushirika wanaoufanya unakuwa ni wa kisasa wenye hadhi kubwa kwa ajili ya kumsaidia Mwanaushirika kama ambavyo Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anataka kuona kwa sababu ndiyo maelekezo aliyowapatia.

“Lakini kingine ni changamoto ya zile barabara za kupita kwenye mashamba yao kama tunavyofahamu mashamba ya Mkonge ni makubwa na tayari serikali tunayo fedha kwa ajili ya kuwapa Bodi ya Mkonge ili waweze kupata hivi vifaa na ni jana tu wameshatuma ile ‘control number’ ili waweze kupata fedha za kuagiza hiyo mitambo ya kuchimba visima kwenye mashamba kujaribu kupitisha zile barabara kuziweka vizuri.

“Kama tunavyosema ushirika ni kwa ajili ya kusaidia kuongeza vipato vyetu na kwa ajili ya kufanya biashara ndiyo maana serikali inawekeza na tukishawekeza hivi na kazi hiyo kubwa ikifanywa na ushirika tunaamini kwamba itakwenda vizuri.

“Kwa hiyo tunaamini kwamba AMCOS zetu hizi tano zinazalisha vizuri kwa tija na katika kiwango kinachojitosheleza ili na sisi kama nchi tuweze kuuza hapa ndani kutumia na kuuza nje ili tupate fedha za kigeni na tuweze kuendelea zaidi,” amesema Dk. Serera.

Naye Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Benson Ndiege amezikumbusha AMCOS hizo kujisajili katika programu ya ‘AMCOS to SACCOS’ inayoitaka kila chama cha ushirika wa mazao kiwe na chama cha akiba na mikopo kwa lengo la kuhakikisha wakulima wanapata namna ya kutunza fedha zao wakati wa mavuno na wakati ambao hawana fedha kwa ajili ya kilimo.

“Kitu kizuri ambacho tumekutana nacho hapa ni kwamba vyama vyote vya mkopo vimefanikiwa kuanzisha SACCOS zao kwa hiyo hii itawasaidia kwenye mambo ya kifedha pale ambapo wanakuwa na changamoto tumewashauri tu sasa wakamilishe usajili.

“Chama cha ushirika tunakwenda kidijitali tuna mfumo wa usimamizi wa vyama vya ushirika katika mfumo huu, wanachama wote na vyama vyote vya ushirika wanatakiwa kujisajili kwa hiyo nachukua nafasi hii kuwasisitiza kwenye maeneo yale ambayo hayajakamilika wahakikishe wamekamilisha usajili wao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Amcos hizo tano, Sedrack Lugendo amesema changamoto za wakulima wadogo ni ukosefu wa mashine za kuchakata mkonge wakulima wengi wanakuwa hawachakati mkonge wao kwa wakati ambapo unakuta mtu anakaa hadi mwaka hajachakata zizlizopo hazitoshelezi na ni mbovu.

“Lakini tunamshukuru Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), alifanya mchakato wa kuleta mashine mpya kwa kila AMCOS ili kila mmoja apate korona yake.

Mhe. Waziri wa Kilimo aliwahi kutuahidi kutatua changamoto hii na leo Naibu Katibu Mkuu ametilia mkazo kwamba wazatalishughulikia jambo hilo mara moja kwa hiyo tuna matumaini makubwa kwamba AMCOS hizi zitawezeshwa mikopo na kupata korona zao binafsi ili kusudi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles