27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Hili la wanafunzi wa UDOM liangaliwe upya.

udom students2KATIKA  kipindi kifupi hapa  nchini yamejitokeza mambo ambayo yamevuta fikra zetu ila yamepita mbele  yetu kama sinema bila kujua ufumbuzi ni nini?  Nikitafakari  wafanyakazi hewa, mauaji lukuki ya kinyama, ukosefu wa sukari nchini, sijui hali sasa ikoje na uendelevu wake ukoje, kulikuwa na sauti za suala la Lugumi, Bunge kutoonyeshwa moja kwa moja, wanafunzi hewa   na mengine mengi  ambayo hayapaswi kupita hivi hivi bila wananchi kujua  mwisho wake. Baada ya hapo limeibuka la wanafunzi wa masomo ya Diploma ya Ualimu  katika Chuo kikuu cha Dodoma.

Kwa muda mrefu sasa tumeshuhudia  jinsi masuala ya elimu  ambavyo yamekuwa yakipelekwa kwa matakwa ya ama Waziri aliyeko madarakani wakati fulani au mkuu wa nchi. Pamekuwa na suala la mitaala kubadilika,  masomo yanayosomwa kubadilishwa bila kuwa na mpango endelevu, aina ya vitabu vya rejea na kiada na kadhalika.

Pia tunakumbuka jinsi ambavyo kukosekana kwa mipango thabiti ya uendelevu wa elimu kuna wakati kumekuwa na ukosefu mkubwa wa walimu kwa ujumla lakini pia walimu wa masomo fulani fulani.

Kipo kipindi palikuwa na upungufu wa walimu wa masomo ya hisabati na fizikia katika shule za sekondari ikabidi wanafunzi waliomaliza kidato cha sita mwaka 1974 baada ya kumaliza kutumikia Jeshi kwa mujibu wa sheria wapelekwe Chuo Kikuu moja kwa moja kwenda kusomea ualimu wa masomo hayo.

Kuna wakati walimu wa shule ya msingi walipungua kutokana na  uandikishwaji wa watoto katika mpango  uliofahamika kama UPE kwamba kila mtoto  mwenye umri wa kwenda shule aende shule. Hapa walipatiwa elimu ya ualimu kwa muda mfupi na kwenda shuleni kufundisha.

Pia kuna wakati upungufu kama huo ulisababisha  mpango  wa wanafunzi wa kidato cha nne kupelekwa katika vyuo na kusoma kwa miaka mitatu na walipomaliza kuwa walimu.

Yote haya yamekuwa yakifanyika kwa njia ya dharura kwa vile inaonekana hatuna mpango kabambe wa uendelevu katika elimu ya ualimu kwa uwiano na wanafunzi wanaongezeka mwaka hadi mwaka. Hasa panapokuwa na ukuzwaji wa uandikishwaji wa wanafunzi kama vile shule za kata zilipoanzishwa haikwenda sambamba na uwepo wa walimu.

Hivi karibuni pametokea utata mkubwa hapa nchini pale wanafunzi  zaidi ya elfu saba waliokuwa Chuo Kikuu cha Dodoma walivyoondolewa chuoni hapo kwa sababu ambazo hadi sasa hatujazielewa vizuri.

Waziri wa Elimu   alielezea bungeni  kuwa wakufunzi wa chuo hicho waligoma na hivyo ikabidi wanafunzi hao wafukuzwe.

Maelezo haya yalishangaza watu wengi kuwa iweje wagome wakufunzi  kisha wanafunzi wafukuzwe? Hii  ilishangaza zaidi kwani njia waliyofukuzwa wanafunzi hao haikuwa na utu kabisa ndani yake kwani hawakupewa muda wa kutosha kujiandaa kuondoka.

Walipewa saa 24 na wengi wao hawaishi hapo Dodoma na walihitaji wapate nauli ili waweze kusafiri kurudi makwao. Hili lilizua tafrani  kubwa bungeni pale Mbunge mmoja alipotoa  rai ya kutaka jambo hilo lipatiwe muda kujadiliwa  jambo lililosababisha wabunge kutoka bungeni pale Naibu Spika alipoipinga rai hiyo.

Wakati bado tunajiuliza maswali  Rais wa Jamhuri  Dk. Magufuli naye akatoa maelezo kuhusu kufukuzwa kwa wanafunzi hao. Maelezo ya  Rais  hayakuhusu walimu waliogoma bali kuwa wanafunzi hao walipelekwa chuoni hapo kinyume na taratibu za kudahili wanafunzi wa chuo.

Walikuwa hawakidhi viwango  vinavyotakiwa kielimu na wengi wao ni ‘vilaza’ na wengine ni watoto wa wakubwa walioingia kwa upendeleo. Katika kujaribu kujiuliza ilikuwaje ikawa hivyo, kuna baadhi ya wanafunzi waliojieleza jinsi walivyopata wito na kupewa nafasi hizo.

Waliojieleza  walisema wanaufaulu wa daraja la kwanza la pili na la tatu na walifaulu masomo ya Sayansi na walikuwa wanasoma Stashahada ya  Ualimu.

Katika mgogoro wote huu muathirika mkubwa ni huyu mwanafunzi kijana wa Kitanzania anayejaribu kupata elimu ili aje kulijenga taifa hili. Maswali kadhaa yameulizwa.

Kwanini maelezo ya suala hili yanakinzana? Hawa wanafunzi kama ni vilaza au la, walifikaje chuoni pale? Ni kosa la nani kwa hawa vijana kuwapo chuoni hapo?  Iwapo Serikali iliyopo sasa iliona mpango huu si sahihi na pamoja na kuwa Serikali iliyopita iliuona kuwa sahihi ni utaratibu gani wa kufaa ungeweza kufanyika bila kuwaathiri vijana hawa ambao wamejikuta katikati ya tafrani hii?  Nimemsikia Rais akisema waangaliwe wenye sifa watafutiwe shule nyingine na wale wasio na sifa waondoke wakatafute kazi nyingine.

Kwa nini hili lisingefanyika kabla vijana hawa kuondolewa kwa njia waliyoondolewa? Hivi  ni kweli  kuwa wote ni vilaza?  Na hata kama walikwenda pasipo na sifa kwa nini wasiondolewe kistaarabu wanafukuzwa kama vile walijipeleka wenyewe pale chuoni?

Ni nani anayeweza kutoa majibu ya maswali haya? Hawa vijana walishaanza chuo na wengine walikuwa mwaka wa pili hata wakipewa nafasi za kuendelea na Kidato cha Tano bado kutakuwa na muda walioupoteza ambao utafidiwa vipi? Ijulikane pia Kidato cha Tano kuna malipo na hakuna mkopo kama ilivyo chuo.

Wazazi ambao walishajipanga tofauti kuna uhakika gani watakuwa na uwezo na utayari wa kuwaendeleza tena vijana hawa? Niliwahi kusikia na kuambiwa msemo kuwa Mkubwa hakosei.

Labda ni kweli  ndio maana naona nitoe rai kuwa suala hili ni suala linalohusu maisha ya mtu. Kila kijana aliyekuwa hapo chuoni ni mtu binafsi mwenye maisha yake na mwenye matamanio na  njozi zake.

Hali kama hii kwa wanafunzi wanaozidi elfu saba ni hatari kuachiwa bila ufumbuzi wa haraka.  Vijana hawa walioonekana wakihangaika na kuzagaa stendi hapo Dodoma na kuona jinsi walivyotendewa katika  kuondolewa katika chuo walichoalikwa  ni fedheha.

Kama baadhi ya wanafunzi hao walivyojieleza inafaa wanafunzi wote warudishwe chuoni. Kama kuna suala la sifa zilizokosewa hilo lishughulikiwe katika ubinafsi wake.

Iwapo walimu wa kuwafundisha hawakuandaliwa waandaliwe pia mara moja. Suala la kusitisha mpango huu lianzie mwaka mpya wa udahili. Hawa wanafunzi waachwe wakamilishe masomo yao.

Wakisoma kwa miaka mitatu iliyosemekana kwa hakika wanaweza kuwa na uwezo wa kupata Stashahada kwani walimu wengi wa Stashahada wamesoma kidato cha tano na cha sita kwa miaka miwili na mwaka mmoja wa ualimu.

Hakutakuwa na hitilafu iwapo watafundishwa vizuri. Kuwaacha hawa wanafunzi au kusema watafutiwe shule inaweza isiwe sawa. Kisaikolojia wanafunzi hawa watakuwa wameathirika hasa kwa muda waliokwisha kuutumia na nafasi watakazokwenda kuchukua.

Mara nyingi tukizungumza masuala kama haya huwa hayaeleweki. Lakini kikubwa tunachoangalia hapa ni kuwa hawa ni watu.Wana hisia na hii ni haki yao kuchukuliwa kama binadamu wenye hisia. Kama kuna makosa yaliyotendeka wao wasibebeshwe huo mzigo.

Pendekezo ambalo tunadhani lingefaa kwa hali ilivyo sasa tukiunganisha alilosema Waziri wa Elimu na alichosema Rais wetu ni kuanza na kutafuta suluhu na walimu waliogoma. Walimu hawa wana sababu zao hivyo zisikilizwe na ufumbuzi upatikane.

Baada ya hapo wanafunzi wenye sifa stahiki warejeshwe chuoni waendelee na masomo yao kama ilivyokuwa imepangwa. Iwapo bado kunaonekana kuna upungufu basi pawepo na njia ya kuhuisha taaluma yao kwa ama kuwa na mafunzo ya ziada au kuongeza muda wa elimu yao. Kuwaondoa chuoni  itakuwa si sahihi  kutokana na sababu nyingi nilizozitoa.

Hali hii pia isifumbiwe macho iwapo haikuwa katika  mpango na kuna mtu tu aliamua kupindisha basi huyo ndiye ashughulikiwe.

Iwapo ilikuwa ni mpango wa Serikali iliyopita kwa vile Serikali  hii iliyopo madarakani si mpya kwa maana ya kuwa watu wote serikalini wamebadilika basi waliokuwa wamesimamia uwepo wa wanafunzi hawa waondoe hofu au woga watoe ufafanuzi na sababu za kuwapo kwa  mpango huo wa elimu.

Jambo hili pia litufundishe kuanza kupanga mipango ya muda mrefu ya elimu na mingineyo na hasa kuwianisha ukuaji wa wanafunzi na kasi ya kufundisha walimu.

Pia tujifunze kuwa ipo haja ya kuwa  na njia sahihi za kukabidhiana madaraka kutoka awamu moja kwenda nyingine.

Mpango uliokuwapo ueleweshwe kwa Serikali mpya. Iwapo haitaafiki basi itafute njia za kuleta mabadiliko ambazo hazitaathiri walioguswa na mpango huo. Kwa hawa walioguswa sasa pawepo na njia za haraka za kurekebisha. Tukumbuke tu kuwa wanafunzi  hawana kosa  kwa kudahiliwa katika mpango huo.

Pia si sahihi wataalamu kulazimishwa kutekeleza mipango wanayoamini kuwa si sahihi. Kazi ya wataalamu ni kusema ukweli wa kitaalamu na iwapo wanasiasa  na watunga sera hawawaelewi ni bora kujiengua badala ya kufanya kitu ambacho kwa taaluma kinaoneka si sahihi  kwani kwa kufanya hivyo ni kuidharaulisha taaluma. Kwa hili la UDOM kuna jambo lakufanya.

Imeandaliwa na DKT Helen Kijo-Bisimba Mkurugenzi  Mtendaji Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles