24.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 19, 2024

Contact us: [email protected]

Ndugu wagombea maiti Muhimbili

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

MWILI wa marehemu Alfredina Mbasha umelazimika kusota katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) baada ya pande mbili za ndugu, kila mmoja kutaka kumzika.

Hali hiyo ilijitokeza jana hospitalini hapo wakati watoto watatu wa marehemu walipokwenda kuchukua mwili wa mama yao na kuambiwa kuwa umezuiwa kwa amri ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira.

Ndugu hao walikuwa wameongozana na mtoto wa marehemu, Eva Kassis ambaye ndiye aliyekuwa akimuuguza mama yake hadi alipofariki dunia Juni 5 mwaka huu, na ndiye aliyekuwa amepewa kibali cha kuuchukua mwili huo.

Akizungumza na MTANZANIA, Eva alisema walifika hospitalini hapo mapema asubuhi kwa ajili ya kuuandaa na kuchukua mwili kwenda kuuzika lakini walishangaa, baada ya kumaliza taratibu zote, walizuiwa kwa madai kuwa

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi alitoa agizo la kuzuia mwili huo.
“Mjomba ndiye ambaye alikuwa hana maelewano mazuri na marehemu mama yetu (dada yake wa kuzaliwa), lakini ameamua kumtumia Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Generali Rwegasira ambaye pia ni ndugu yetu ili kutunyanyasa.

“Jana tulifika mapema asubuhi tukafanya maandalizi yote na kibali tulishapewa wakati tukijiandaa kuondoka, mmoja wa watumishi wa mochwari alituambia mwili umezuiwa kwa amri ya katibu mkuu,” alisema Eva.

Alisema agizo hilo liliwashtua na kuwasikitisha kwa vile tayari walikwisha kutumia gharama kubwa na tayari gari la kuubeba mwili wa marehemu kwenda makaburini lilikuwa limewasili katika eneo hilo pamoja na sanduku la kuuweka mwili huo.

“Ugomvi huo ulianza baada ya babu kufariki dunia. Wakati babu alipokuwa anaumwa alilazimika kuuza shamba lake ili atibiwe mama yangu ndiyo aliyemuuguza babu. Fedha zile ziligawanywa kwa ajili ya matibabu, nyingine walinunua eneo kwamba akipona afikie kwake.

Hata hivyo mjomba alianza kudai fedha za babu, alifungua kesi mahakamani na mama akafungwa kifungo cha nje miaka sita,” alisema.
Hata hivyo, jana Jenerali Rwegasira alifika katika eneo hilo akiwa ameongozana na mjomba anayedaiwa kuzuia mwili.
Aliwaleza ndugu hao kuwa walitoka katika kikao maalum na mwanasheria wa hospitali hiyo kutafuta suluhu ya suala hilo.

“Jamani sijazuia maiti mimi, kule kwa mwanasheria tumeambiwa turudi katika ofisi ya serikali ya Mtaa Kiwalani tupewe barua ili tuje tupatiwe mwili tukazike sasa tuelekee huko,” alisema Katibu Mkuu huyo.

Hata hivyo kauli hiyo iliwaudhi ndugu hao na kumjibu hawaendi huko na kwamba watakesha katika eneo hilo la chumba cha maiti kuhakikisha mwili wa ndugu yao hauondolewi na mtu yeyote.
Naye mume wa marehemu, Kassis Mwakabonja alisema walipanga kumzika mkewe jana katika makaburi ya Chang’ombe.

Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja wa hospitali hiyo, Aminiel Aligaesha alisema wamelazimika kuzuia mwili huo hadi ndugu hao watakapopatana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles