Na MWANDISHI WETU
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewataka wahandisi washauri nchini, kutotumia vibaya vyeo na dhamana walizonazo kwa kuwalazimisha wakandarasi kununua bidhaa sehemu wanazotaka wao.
Pia, amewataka watendaji wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, wakurugenzi wa halmashauri na majiji nchini pamoja na wahandisi washauri, kutumia mabomba yanayozalishwa na viwanda vya ndani kwa kuwa yanakidhi viwango vya ubora.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo juzi wakati wa uzinduzi wa kiwanda cha kutengeneza bidhaa za plastiki cha Lodhia, akiwa katika siku yake ya pili ya ziara yake ya kikazi mkoani Arusha.
“Serikali inalenga kumaliza tatizo la ajira hasa kwa vijana kwani Serikali peke yake haiwezi kuwaajiri watu wote.
“Viwanda pekee ndivyo vyenye uwezo wa kuzalisha ajira nyingi na jukumu letu ni kuviunga mkono viwanda hivyo.
“Binafsi sioni sababu ya halmashauri na wakandarasi kununua mabomba kutoka nje ya Arusha au nje ya nchi wakati bidhaa hizo zinazalishwa na wawekezaji ndani ya mkoa huo na zinakidhi viwango vya ubora.
“Pamoja na hayo, nawataka watumishi wa kiwanda hiki mfanye kazi kwa weledi na uaminifu mkubwa ili muweze kuzalisha bidhaa nyingi zaidi na hatimaye kuongeza ajira,” alisema Waziri Mkuu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Sailesh Pandit, alisema moja ya changamoto zinazowakabili kiwandani hapo ni kushindwa kuuza bidhaa wanazozalisha katika miradi mikubwa ya maji inayotekelezwa mkoani Arusha.
“Pamoja na kuwa na bidhaa zenye viwango vya ubora vilivyothibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na ISO, tunashindwa kuuza kutokana na hujuma tunazofanyiwa na baadhi ya wahandisi wa halmashauri na washauri elekezi wa miradi ya maji mkoani hapa.