30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

NIYONZIMA KUFUATA  NYAYO ZA RONALDO?

Na  ZAINAB IDDY-DAR ES SALAAM


haruna-niyonzimaALIKUJA akawakuta, wamemkuta na kumwacha akiendelea kutesa. Ni kiungo mchezeshaji wa klabu ya Yanga, Haruna Niyonzima.

Maisha ya mchezaji huyo ndani ya klabu hiyo, yanaweza kufananishwa na staa wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo, ambaye alitua Hispania mwaka 2009 akitumia miaka saba kusakata soka lake ndani ya dimba la Santiago Bernabeu na kutwaa tuzo mbalimbali sambamba na mataji.

Kulingana na sera ya Madrid ya kusajili wachezaji wa bei mbaya ‘Galacticos’, licha ya kumsajili Ronaldo kwa gharama iliyoandika rekodi ya usajili ghali duniani, bado waliongezwa mastaa wengine kutoka Ulaya na kwingineko. Lakini bado Ronaldo ameendelea kutesa, hadi sasa akiwa sambamba na mchezaji wa mwisho kununuliwa kwa bei mbaya zaidi, Gareth Bale.

Katika miaka yote hiyo ya kuletewa mastaa mbalimbali waliotabiriwa kuvunja ufalme wake, Ronaldo amedhihirisha kuwa yeye ndiye mfalme wa Madrid, akiisaidia timu hiyo kunyakua mataji, yakiwemo mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na moja la La Liga, huku akijikusanyia tuzo binafsi za kutosha, zikiwemo za ufungaji bora (tatu) na nyinginezo za ligi hiyo.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Niyonzima, aliyetua Yanga 2011 akitokea katika klabu ya APR ya Rwanda.

Kuanzia hapo hadi kufikia sasa, Niyonzima amekuwa mchezaji wa kigeni aliyedumu zaidi katika klabu ya Yanga, wakati wenzake ambao walitua pamoja naye, kipa Yaw Berko (Ghana ), Tonny Ndolo (Uganda ), Keneth Asamoah (Ghana) na Davis Mwape kutoka Zambia wakicheza na kuondoka kwa nyakati tofauti na kumuacha akiwa anaendelea kukipiga kwa mabingwa hao wa ligi mara 26.

Mbali na kutua na wanandinga hao, wapo ambao walitua na kuondoka, wakiwemo Wabrazil Genilson Santos ‘Jaja’, Andrey Coutinho na Emerson Rouqe, Mliberia Kpah Sherman na Waganda wawili, Emmanuel Okwi na Amis Kiiza.

Akiwa na kikosi cha Jangwani, Niyonzima ambaye ni mzaliwa wa mji wa Gisenyi, Rwanda, ameisaidia Yanga kutwaa makombe takribani saba yakiwemo ya Ligi Kuu, Ngao ya Jamii, Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lakini pia akiisaidia kufika hatua ya robo fainali katika michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika mwaka huu.

Thamani yake inapanda kila uchao

Mengi yamesemwa kuhusu Niyonzima, lakini ukweli unabaki kuwa yeye ni mmoja wa wachezaji wa kigeni waliovuna mamilioni katika soka la Tanzania, kutokana na kupanda kwa thamani yake kila dirisha la usajili linapokaribia.

Kwa hesabu za haraka haraka bila kujumlisha posho na marupurupu mengine, Niyonzima amevuna zaidi ya Sh milioni 680 katika malipo ya usajili na mishahara yake.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana ndani ya Yanga, Niyonzima aling’olewa APR kwa dau la dola za Marekani 30,000 ambapo alipewa mkataba wa miaka miwili na kuahidiwa mshahara wa dola za Marekani 1,500.

Mwaka 2013, dau lake lilipanda baada ya kuongezwa mkataba wa miaka miwili tena kwa kitita cha dola elfu 75 na mshahara wa dola 2,500 kwa mwezi.

Mwaka 2015, wakati wengi wakiamini uwezo wake umepungua, Niyonzima alitikisa kiberiti kwa kuuambia uongozi kwamba yupo tayari kutua Simba au Azam, jambo lililoifanya Yanga kukubali kumpa mkataba wenye maslahi ya kutosha ambapo walihakikisha kiungo wao huyo haondoki kwa kumwongezea mshahara wa dola za Marekani 3,000.

Licha ya misukosuko aliyokutana nayo ndani ya Yanga, ikiwemo uongozi kuamua kuvunja mkataba wake kabla ya kutengua kauli hiyo na mapungufu yake mengine ndani na nje ya uwanja, Niyonzima amekuwa akipanda dau kwa sababu ya kujiamini na kutambua kuwa njia ya kupigania maslahi yake ni kuonesha kiwango cha hali ya juu, kuwafunga midomo wale wasiohitaji kumuona akiendelea kuitumikia Yanga.

Ili kuonyesha umuhimu wake ndani ya Yanga msimu huu, Niyonzima ameendelea kuwa mwiba kwa wapinzani kiasi cha kuwafanya mashabiki na mabosi wa timu hiyo, kujiapiza kuwa mkataba wake utakapomalizika hawatokubali kumuacha aondoke kirahisi.

Kwa kiwango chake cha sasa kinachopelekea baadhi ya mashabiki wa Yanga kutembea vifua mbele, ni wazi kuwa dau lake litapanda maradufu, kwani hakuna ambaye mpaka sasa amesimama na kudai jamaa hafai kuendelea kuichezea Yanga.

Umahiri wake wa kuichezesha timu kwenye eneo la kiungo, unaifanya Yanga ifikiri mara mbili suala la kumtema na dalili zinaonesha wazi kuwa huenda akaendelea zaidi kukipiga ndani ya klabu hiyo, huku ikiwa siku atakayoondoka bado haijajulikana.

Mwenyewe atoa neno

Niyonzima anasema kuwa licha ya kuwa yeye ni raia wa  Rwanda, lakini si kitu kibaya akijiita Mtanzania kutokana na kuishi muda mrefu  hapa nchini hapa na kuzitambua mila na tamaduni nyingi za nchi hii.

“Nina muda mrefu hapa Tanzania na hii ni kwa sababu ya kazi yangu ya soka, niwashukuru sana Wanayanga wanaoutambua umuhimu wangu ndani ya kikosi, kiasi cha hata ikitokea nikitaka kuondoka, wao ndio wanapigania nibaki.

“Shukrani nyingi ziuendee uongozi wa Yanga. Kama wasingenisajili, nisingefikia ubora nilionao. Nawaahidi kuendelea kuwa pamoja nao katika kila hatua ili kuipa mafaniko timu yetu,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles