22.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

AJALI YA CHAPECOENSE INAPOKUMBUSHA MACHUNGU

JOSEPH HIZA NA MTANDAO


chapecoenseBADO ni wiki ya simanzi kwa wadau wa soka nchini Brazil na duniani kwa ujumla kutokana na tukio la ajali ya ndege iliyotokea mwanzoni mwa wiki iliyopita na kuua watu 76 papo hapo.

Ndege hiyo ilikuwa imewabeba watu 81, ikiwamo kikosi cha moja ya klabu kubwa za soka nchini Brazil, Chapecoense, ilianguka wakati ikikaribia kutua katika jiji la Medellin nchini Colombia majira ya saa sita usiku.

Polisi nchini Colombia walisema watu watano walinusurika lakini wengine wote walikufa katika ajali hiyo.

Ndege hiyo ya kukodishwa ilikuwa safarini kutoka Brazil ikipitia Bolivia na ilikuwa imewabeba wachezaji, maofisa wa timu ya Chapecoense pamoja na wanahabari waliokuwa wakienda kuripoti mechi inayoihusu.

Video iliyopo katika ukurasa wa facebook wa Chapecoense ilionesha kikosi cha timu hiyo kikiwa tayari kwa safari kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Guarulhos mjini Sao Paolo.

Na ilipotua Bolivia, ilipiga picha ya pamoja kabla ya kuruka kuelekea Colombia kwa ajili ya mechi hiyo kubwa kabisa katika historia ya klabu hiyo, fainali ya Copa Sudamerica.

Michuano hiyo ina hadhi sawa na ile ligi ya vilabu Ulaya, UEFA Europa.

Lakini safari yao katika hali itakayochukua muda mrefu kusahaulika katika ulimwengu wa soka,  iliishia vibaya baada ya kuanguka milimani zikiwa zimebaki dakika tano tu kutua kwenye uwanja wa ndege wa Jose Maria Cordova de Rionegro, mjini Medellin.

Klabu hiyo ilikuwa imepangiwa kucheza mechi ya fainali ya michuano hiyo na timu ya Atletico Nacional ya Medellin.

Mechi ya awamu ya kwanza ya kombe hilo la pili kwa umuhimu Amerika Kusini, ilikuwa imepangwa kuchezwa Jumatano wiki iliyopita.

Kutokana na ajali hiyo, Shirikisho la Soka la Amerika Kusini (Conmebol) limesema limesitisha shughuli zake zote kwa sasa.

Kwa mujibu wa maofisa, ndege hiyo chapa Avro RJ85 ya muundo wa British Aerospace 146 ambayo ilikuwa ikitumiwa na Shirika la Ndege Lamia la Bolivia, iliyobeba wafanyakazi tisa, ilikumbwa na tatizo katika mfumo wake wa umeme wakati ikielekea Bolivia.

Maofisa wanasema ilianguka milimani na kukatika vipande viwili na ripoti zinasema rubani aliizungusha angani katika harakati za kuchoma mafuta kabla ya kutua.

Timu hiyo kutoka jiji dogo la Chapeco, kusini mwa Brazil ilikuwa katikati ya kilele cha mafanikio msimu huu.

Ilipanda Ligi Kuu mwaka 2014, mara ya kwanza tangu miaka ya 1970 na ilifika fainali ya Kombe la Sudamericana wiki iliyopita baada ya kuilaza San Lorenzo ya Argentina.

Mechi iliyokuwa ichezwe Jumatano usiku ilikuwa ikitazamwa kuwa kubwa zaidi katika historia ya klabu hiyo.

 

Iliwabeba akina Messi

Tukio hilo limetokea siku 20 tu tangu ndege hiyo hiyo isafirishe timu ya taifa ya Argentina, ikiwa na wachezaji nyota kama vile Lionel Messi na Angel Di Maria na wengine wengi.

Iliwabeba kuwapeleka mjini Belo Horizonte, Brazil, ambako walicheza na Brazil katika hatua ya makundi ya Kombe la Dunia 2018.

Picha za kusikitisha zilionekana mitandaoni zikionesha wachezaji wa timu hiyo waliobaki nyumbani wakiwa wameketi katika chumba cha kubadilisha nguo cha klabu hiyo wakiwa katika huzuni kubwa.

Aidha ,picha tofauti zilionesha wachezaji wawili, mlinzi Alan Ruschel na golikipa Danilo Padilha, wakijipiga picha wakati wa safari ya kutoka Brazil, huku Ruschel (27) akiwaambia mashabiki: ‘Tunakuja Colombia.’

Wote Ruschel na Danilo walitoka hai kutoka mabaki ya ndege, lakini Danilo alifariki dunia baadaye akitibiwa hospitalini.

Golikipa Jacson Follmann, mlinzi Helio Hermito Zampier Neto pamoja na abiria Rafael Correa Gobbato na Ximena Suarez walinusurika katika ajali hiyo, kwa mujibu wa maofisa.

Gazeti la Telemundo Deportes liliandika katika akaunti yake ya Twitter kwamba Ruschel ameathiriwa na mshtuko, lakini ana fahamu na anazungumza. Aidha, ameomba aruhusiwe kukaa na pete yake ya harusi na awaombee jamaa zake.

Kuna ripoti kuwa timu hiyo ilibidi ibadili ndege yao ya awali na kupanda ndege hiyo iliyoanguka, baada ya mamlaka za anga za Brazil kuwazuia kupanda ndege ya kukodi.

Maofisa walifichua kuwa miili 25 tayari imepatikana, timu za uokoaji zililazimika kusitisha opereshani zao kutokana na mvua nzito katika eneo hilo la milima.

Maofisa wa klabu hiyo ya Chapecoense wametoa taarifa wakisema: “Tunamuomba Mungu awe na wachezaji, maofisa, wanahabari na wageni wengine watu ambao walikuwa wameandamana na msafara wetu.”

Wamesema hawatatoa taarifa nyingine hadi ibainike kiwango kamili cha mkasa huo.

Meya wa mji ulio karibu wa La Ceja amethibitisha kwamba mchezaji mmoja wa miaka 25 ni miongoni mwa manusura.

Meya wa Medellin, Mayor Federico Gutierrez amesema ajali hiyo ni “janga kubwa”.

Marubani na wafanyakazi wa ndege wote walikuwa raia wa Bolivia, huku abiria wote wakitokea Brazil na karibu 40 wakiwa sehemu ya msafara wa Chapecoense.

Hao ni pamoja na wachezaji 20, Kocha Caio Junior na wasaidizi wake wanne.

Rais wa klabu na makamu wake walikuwa miongoni mwa waliokuwamo.

 

Nyota na klabu zawalilia

Nyota wa Brazil na Barcelona, Neymar aliongoza wanasoka nyota duniani kutoa pole na salamu za rambirambi kwa waathirika wa ajali hiyo.

“Ni ngumu kuamini janga hili, ni ngumu kuamini tukio hili, ni ngumu kuamini ndege ilianguka, ni kuamini wachezaji, binadamu walikuwa katika ndege hii, ni nigumu kuamini kwamba watu hawa wameziacha familia zao,” aliandika katika akaunti yake ya Instagram.

“Leo hii dunia inaomboleza, lakini mbingu zinashangilia kuwapokea mabingwa. Mawazo na hisia zangu ziko pamoja na familia na marafiki wa waathirika,” aliandika.

Wachezaji wengine walioomboleza msiba huo mkubwa kwa familia ya soka ni pamoja na nahodha wa England, Wayne Rooney, nyota wa zamani wa Real Madrid na Ureno, Luis Figo, golikipa wa Porto, Iker Casillas, mfalme wa soka nchini Brazil, Pele, pamoja na Rais wa FIFA, Gianni Infantino.

Wengine ni pamoja na nahodha wa zamani wa Ujerumani, Michael Ballack.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, mashabiki wa klabu ya Chapecoense nchini Brazil zaidi ya 100,000 walikutana katika uwanja wa klabu hiyo na kufanya maombolezo usiku kucha.

 

Ajali nyingine katika historia ya soka

Klabu ya Manchester United, ambayo ilipoteza wachezaji wanane Februari 1958 wakati ndege yao ilipoanguka wakati ikiruka kutoka uwanja wa ndege wa Munich, Ujerumani iliandika katika ukurasa wake wa Twitter: Mawazo ya kila mtu katika Manchester United yako kwa Chapecoense na wote walioathirika na janga hili nchini Colombia.

Ajali hiyo ya Munich iliyoikumba klabu hiyo ya England ni moja ya nyingi zisizosahaulika katika ulimwengu wa soka, nyingine ikiwa ile iliyohusisha timu ya taifa ya Zambia mwaka 1993.

Kikosi hicho cha Zambia kikiwa na watu 30, wakiwamo wachezaji 18, walikufa baada ya ndege yao ya kukodi ya Jeshi la Anga la Zambia kuanguka katika pwani ya Gabon, baada ya kuruka. Ilikuwa njiani kuelekea Senegal kwa mechi ya kufuzu ya Kombe la Dunia.

 

Kupewa ubingwa?

Baada ya tukio hilo kutokea, kulikuwa na ripoti kuwa Chapecoense itatawazwa taji la ubingwa wa Copa Sudamerica kipindi cha siku chache zijazo.

Kwa mujibu wa mwandishi wa michezo wa Brazil,  Thiago Suman, waliokuwa wacheze nao, Atletico Nacional ya Colombia inaaminika kupanga kuwasilisha maombi kwa Shirika la Soka Amerika ya Kusini ili kuachia taji la ubingwa kwa Chapecoense kwa ajili ya kuwaenzi wachezaji waliofariki ili kuonesha mshikamano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles