WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amemwagiza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, kuboresha upatikanaji wa huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa kuhakikisha inakuwa na dawa na vifaa tiba vya kutosha.
Alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki alipotembelea hospitali hiyo akiwa kwenye ziara ya kukagua maeneo ya kutolea huduma za jamii mjini Dodoma.
Alisema Serikali ikishirikiana na uongozi wa mkoa huo katika kumaliza changamoto zinazoikabili hospitali hiyo, manispaa nazo zina jukumu la kuboresha utoaji wa huduma za afya katika zahanati na vituo vya afya.
“Waziri wa Afya atawajibika kuimarisha hospitali ya mkoa, manispaa waimarishe huduma katika zahanati zote na vituo vya afya ndani ya mkoa kwa kuziwezesha kuwa na majengo ya kutosha, kuongeza idadi ya watumishi na kuhakikisha zinakuwa na dawa na vifaa tiba,” alisema.
Aliwataka watumishi wa hospitali hiyo kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu na isitokee watu wakakosa dawa au vipimo kwa sababu mmoja wao amechukua na kupeleka kwenye duka lake binafsi.
Pia alimwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. James Kiologwe, kutafuta vijana watakaoweza kusafisha na kutengeneza bustani ya maua kwenye eneo lililoko karibu na uzio wa hospitali hiyo ili liwe na mandhari ya kuvutia.
Awali, Kiologwe aliiomba Serikali kupandisha hadhi hospitali hiyo na kuwa ya kanda kwa sababu mbali ya mkoa wa Dodoma, hospitali hiyo inahudumia wagonjwa wengine kutoka mikoa ya Iringa, Tabora, Singida na Manyara.
Akizungumzia upatikanaji wa tiba wakati Serikali imeanza kuhamia Dodoma, Dk. Kiologwe alisema mkoa huo unaweza kukabiliana na ongezeko la watumishi kwani una hospitali tano ambazo zina madaktari bingwa wa fani mbalimbali.
“Tunazo hospitali tano ambazo ni Benjamin Mkapa, Mirembe, DCMC, St. Gemma na hii ya ya Rufaa ya Mkoa zenye uwezo wa kutoa huduma za upasuaji, huduma kwa mama na mtoto, magonjwa ya moyo, mishipa, figo na saratani na huduma za mionzi,” alisema.
Katika hatua nyingine, Dk. Kiologwe alisema hospitali hiyo imehudumia wagonjwa wa nje 158,375 waliopatiwa huduma katika hospitali hiyo katika kipindi cha Julai mwaka 2015 hadi Juni 2016, sawa na wastani wa wagonjwa 13,198 kwa mwezi.