24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wayne Rooney apewe muda wa kupumzika

wayne-rooneyNA ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM

KWANINI kila siku Wayne Rooney? Hivyo ndivyo unavyoweza kuuliza baada ya nahodha huyo wa Manchester United kuonekana tatizo ndani ya kikosi cha timu hiyo licha ya kuwa  benchi katika michezo kadhaa.

Kila kona Rooney, kila siku Rooney likitokea kosa uwanjani hata kama yupo benchi utasikia ooh Rooney, Mpeni nafasi apumue.

“Wote tunajitahidi kumsaidia Rooney kwa kadri tuwezavyo ili arejee katika kiwango chake,” alieleza David Moyes wakati akifundisha timu ya Manchester United.

Kocha huyo pia kwa vipindi tofauti alisikika akimzungumzia nyota huyo katika mtazamo tofauti: “Unatakiwa kuelewa kilichopo kwa kiungo huyo kwani anatakiwa kuheshimiwa na kwa sasa anahitaji nafasi ya kupumua kwani mambo yalivyo najua atakuwa amechanganyikiwa.”

Huyo ni Moyes wa Manchester United? Hapana  ni wa Eveton ambapo wakati huo Rooney akiwa na umri wa miaka 17 aliposhindwa kuendana  na mfumo wake baada ya kucheza michezo 11. Sasa ametimiza  michezo   710 lakini  hakuna kilichobadilika  mwendo ni  ule ule wa kumnyooshewa kidole.

Ndio Manchester United imeonekana kuwa vizuri hata bila ya Rooney katika michezo kadha lakini pia bila ya Henrikh Mkhitaryan ambaye amedaiwa kushindwa kufanya vema katika michezo kadhaa iliyopita na pia bila Daley Blind.

Ni Manchester ambayo haitaki kusikia wala kuona uwepo wa Luke Shaw, beki ya kushoto huku  ikipiga kelele kuhusu Anthony Martial na kumponda  Marouane Fellaini  kwa makosa ya kizembe.

Hivyo si Rooney pekee aliyekosa michezo kadhaa ukiwamo dhidi ya  Leceister City ambao timu hiyo ilishinda mabao 4-1 bali Mkhitaryan, Shaw, Martial na  Fellaini hawakuanza kikosi cha kwanza katika mchezo huo, ingawa Blind aliingia na kucheza kama mkoba.

Lakini ghafla kukosekana kwa Rooney kumeonekana  ndio kumekuwa suluhisho la tatizo la muda mrefu kwa timu hiyo ikiwa pamoja na michezo mitatu iliyopita waliyopoteza mfululizo.

Kocha Mkongwe wa Italia, Enzo Bearzot ‘Sempre Butcher,’ aliwahi kusema kuwa enzi zake wakati beki ya timu ya taifa ya England ikikosolewa kila wakati lazima litajwe jina lake Butcher.

Na sasa ‘Sempre Rooney’ kila wakati Rooney, kama England ikishindwa kuonesha kiwango bora zigo la lawama anadondoshewa Rooney, kama  Manchester United ikipoteza basi kidole kwa  Rooney.

Rooney alianza msimu akiwa na kiwango bora huku akifanikiwa kufunga bao licha  ya kusemwa vibaya na kuonekana kuwa hana msaada wowote katika kikosi cha kocha Jose Mourinho.

Nyota huyo pia alikuwa mwiba katika mchezo dhidi ya Hull City pia katika mchezo dhidi ya Southampton ambapo pasi yake ilimfanya Zlatan Ibrahimovic kuonekana shujaa baada ya kufunga bao.

Lakini wakati kiwango cha nyota huyo kinaposhuka na kushindwa kuonesha ubora wake kila kitu kinamwelekea yeye.

Rooney amekuwa kama mtoto mtukutu kila wakati kwa kuonekana kama chanzo cha tatizo, pasua kichwa kuliko alivyo ndani ya timu hiyo.

Mkongwe wa zamani wa klabu hiyo, Gary Neville anasema kuwa hali hiyo inamkuta nyota huyo akiwa amecheza michezo 721 akiwa bado hajafikisha hata umri wa miaka 31.

Ikiwa hivyo baada ya miaka 10 hali itakuwaje kwa nyota huyo? lakini kwa umri wa miaka 30 hakutakiwa kuwa katika hali aliyonayo sasa.

Si mchezaji wa ‘part-time’ ni kioo kwa kinda wa timu hiyo, Marcus Rashford ambaye amekuwa moto huku akiwa bado anahitaji msaada mkubwa wa kufanikisha safari yake ya mafanikio kutoka kwa nahodha huyo.

Hata hivyo huenda Mourinho alimweleza Rooney ameshuka kiwango na anatakiwa kupambana ili kulinda nafasi yake kama nahodha wa timu hiyo.

Ushauri huo unaonekana kukubaliwa na kiungo huyo akiamini  atarejea katika kikosi hicho.

Wakati hayo yakitokea, mchezaji wa zamani wa timu hiyo Paul Scholes ameibuka na kusema kuwa Mourinho huenda akamkutumia Rooney katika michezo mkibwa kama vile dhidi ya Liverpool, Chelsea, Manchester City na Arsenal.

Scholes anaaamini kuwa Rooney hawezi kuendelea kuwekwa benchi katika timu hiyo kwani anamchango mkubwa uwanjani.

“Namjua kwa kuwa nimewahi kucheza naye ni mchezaji hasiyependa kuwa nyuma akishuhudia timu yake ikipotea uwanjani.

“Rooney ni mchezaji mwenye uwezo wa kupambana na kutoa hamasa kwa wengine hivyo ni aina ya mchezaji ambaye Manchester United inamuhitaji kwa sasa,”anasema Scholes.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles