Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama amewataka wananchi kuondoka katika maeneo hatarishi ili kujikinga na mafurikio ya mvua za vuli zinazoendelea kunyesha.
Mhagama ameitoa kauli hiyo leo Aprili 12,2024 alipotembelea na kujionea maeneo yaliyokumbwa na mafuriko ya mvua katika Halmashauri ya ya Mlimba mkoani Morogroro jana Aprili 11, ambapo amewaomba wananchi kuendelea kufuatilia na kusikiliza ushauri wa Serikali.
“Niwaombe wananchi tuendelee kushikamana ili kupambana na majanga ya mvua na mafuriko, ambayo yameleta kadhia kubwa sana kwa wananchi.
“Serikali imetengeneza Mpango wa Dharura wa kukabiliana na mvua za El Nino na mvua za masika, ambapo itafanya kila linalowezekana kuzuia madhara yasitokee hasa maisha ya Watanzania,” amesema Mhagama.
Ameongeza kuwa mafuriko ya maji yamesababisha udongo kumomonyoka na kuharibu miundombinu ya reli na kuleta madhara mengine mengi na kuwaomba wananchi wa Mlimba kuendelea kuangalia na kusikiliza ushauri wa Serikali.
“Serikali itaendelea kuhakikisha inapambana dhidi ya magonjwa ya mlipuko na uhaba wa chakula na madhara mengine ambayo yameathiri wananchi, serikali itakuwa pamoja na ninyi katika kutatua kadhia hizo,” amesema Waziri Mhagama na kuongeza:
“Niwaombe wananchi tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu hali iliyopo mbele yetu iweze kupita kwa haraka na ipite kwa usalama mkubwa,” amesema.
Ameeleza katika utabiri wa hali ya hewa unaoendelea kutolewa unaonesha mvua hizi zinaendelea kunyesha hivyo ni vyema wananchi wakaendelea kuchukua tahadhari.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dustan Kyobya amesema changamaoto ya Mawasiliano ya barabara kwa watu wa Masagati na Utengule kwao wamekuwa kisiwa kutokana na miundombinu ya barabara kutopitika, lakini pia mawasiliano kati ya jimbo la Ifakara na Mlimba ambazo zinatengeneza wilaya ya kilombero nayo ni magumu.
“Nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuma ndege kwa ajili ya kuokoa watu waliokwama na kuruhusu treni ya Mwakyembe kuanza kubeba abiria ili kurahisisha mawasiliano,” alisema Mkuu Kyobya.
Awali, Mkazi wa Mlimba, Zainabu Makenjula aliiomba Serikali kushughulikia swala la barabara kwa wakati ili kurahisisha mawasiliano na kuwezesha wananchi kuendelea na shughuli za uzalishaji kwa sababu kuna maeneo magari wala pikipiki haviwezi kupita.