Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
Wauguzi saba wanatumikia adhabu ya vifungo jela katika mahakama mbalimbali nchini baada ya kuthibitika kughushi vyeti vya kitaaluma. Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Lena Mfalila amesema hayo leo jjini Dar es Salaam, katika semina ya siku moja kwa waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya kongamano la kisayansi la wauguzi na wakunga linalotarajiwa kufanyika April 4-7, mwaka huu mkoani Dodoma. “Tumekuwa tukipokea malalamiko ya wananchi na tunachukua hatua, 2016 muuguzi mmoja wa Temeke alifungiwa leseni na tukamnyang’anya vyeti vyake baada ya kumkuta na hatia na baada ya adhabu kuisha tulimrejeshea. “Wengine walipatikana na hatia na kufungwa kwa nyakati tofauti, pamoja na hayo baraza tumeendelea kuhakikisha tunasimamia maadili ya wauguzi na wakunga ili kuhakikisha mama na mtoto wanapata huduma bora,” amesema. Awali, Mkurugenzi wa Idara ya Uuguzi na Ukunga wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Gustav Moyo amesema kazi ya Uuguzi na Ukunga ni ngumu hata hivyo wahusika wanapaswa kuendelea kutoa huduma kwa kuzingatia maadili ya kitaaluma.