Na Elizabeth Kilindi,Njombe
ZAIDI ya watu 75,000 mkoani Njombe, wanadaiwa kuishi na maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Ukimwi (VVU), kati yao 48,000 ndiyo waliojiunga kupata huduma za tiba na matunzo.
Lakini wengi wao, wakiwa ni wanawake, huku wanaume 27,00 hawajui hali zao.
Akizungumza juzi wakati wa uzinduzi wa kampeni ya furaha yangu iliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Bakita, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka alisema wanaume ambao hawajui hali zao za maambukizi wako katika hatari ya kuambikiza watu wengine.
Alisema kupima na kuanza tiba matunzo mapema husaidia kuboresha hali ya afya na kupunguza uwezo wa kuambukiza wasio na maambukizi.
Alisema mkoa kwa kushirikiana na wadau unatoa huduma za VVU na Ukimwi katika vituo 237, vinatoa huduma ya mama na mtoto na vituo 62 vikiwa vinatoa huduma tiba na matunzo.
“Vituo hivi havitoshi, kuna wengine wanasafiri umbali mrefu kufuata huduma hii, nitumie nafasi hii kuagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi kuongeza vituo ikiwezekana kila kata mpango huu ukamilike haraka”alisema Ole Sendeka.
Alisema hadi mwishoni mwa Machi, mwaka huu,wanaume 16,734 pekee walikua wanatumia dawa za kupunguza makali ya VVU,wakati wanawake walikuwa 31,266.
“Wanaume tunajiita majasili hebu kwenye hili tuonyeshe ujasili wetu tulapime ili tujue hali zetu”alisema Ole Sendeka.
Kampeni ya Furah Yangu,Pima,Jitambue,Ishi, inahamasisha mkakati mpya wa Serikali wa upimaji wa VVU na kuanza kutumia ARV mapema.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe,Dk. Manyanza Mponeja alisema wanaume ambao kiwango chao cha upimaji kiko chini kwa asilimi 45.3, ukilinganisha na wanawake ambao ni asilimia 55.9.
“Kuna umuhimu sasa wa kuwahamasisha wanaume kupima na magonjwa mengine na ninawaomba wanawake waunge mkono kwa kuwa tayari mmeonyesha mfano mzuri wa kujali afya zao”alisema Mponeja.