27.3 C
Dar es Salaam
Monday, December 4, 2023

Contact us: [email protected]

DC AONYA WANAOINGIZA VIUATILIFU NCHINI

Na FLORENCE SANAWA- TUNDURU

MKUU wa Wilaya (DC) ya Tunduru, Mkoa wa Ruvuma, Juma Homera, amepiga marufuku uingizwaji wa viuatilifu wilayani humo kutoka nchini Msumbiji.

Akizungumza na wakulima wa kata za Nalasi, Lukumbule, Mtina, Ligoma na Misechela wilayani hapa wakati wa ziara ya kuhamasisha usambazaji wa viuatilifu vya kukinga na kuzuia magonjwa ya korosho, Homera alisema atakayekamatwa akiingiza viuatilifu hivyo atachukuliwa hatua kwa sababu huo ni uvunjifu wa sheria.

Alisema kwamba, Serikali inapinga uingizwaji wa viuatilifu hivyo kwa sababu vinaingizwa nchini bila kufuata utaratibu na vinaweza kuwa na madhara katika korosho.

“Kuna viuatilifu vinaingizwa nchini kutoka Msumbiji vikiwa vimeandikwa Kireno badala ya Kiswahili au Kiingereza ambazo ndizo lugha tunazotumia.

“Kwa hiyo, Serikali kupitia Bodi ya Korosho Tanzania haitaruhusu viuatilifu hivyo viendelee kutumika nchini na atakayekamatwa navyo, ajue atachukuliwa hatua kwa sababu bodi ya korosho imeleta pembejeo za kutosha na zimesambazwa kwa wakulima.

“Sasa  inakuwaje mkulima akanunue pembejeo zilizoandikwa lugha ambayo haielewi bila kujua kama kuna athari zozote zinaweza kujitokeza kwenye zao la korosho, hili hatulikubali,” alisema Homera.

Naye Mkulima wa korosho katika Kata ya Misechela, Salum Hamis, alisema wamekuwa wakitumia viuatilifu kutoka nchini Msumbiji kwa kuwa vinavyoletwa na Serikali vimekuwa vikichelewa kuwafikia na kuhatarisha mazao yao.

Kwa upande wake, Meneja wa Bodi ya Korosho Tanzania, tawi la Tunduru, Shauri Mokiwa, alisema Serikali imeleta viuatilifu vitakavyowawezesha wakulima kupata mafanikio kupitia zao la korosho.

“Lengo la bodi ni kuwahudumia wakulima wa korosho kwa kuhakikisha wanapata viuatilifu kwa wakati mwafaka, vikiwa salama na kuwapa elimu ya matumizi sahihi ili kuwawezesha kuimarisha uzalishaji na kukuza kipato chao na cha Taifa kwa ujumla,” alisema Mokiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles