Na Ashura Kazinja – MOROGORO
WATU 11 wamefariki dunia mkoani Morogoro kwa kuangukiwa na ukuta wa nyumba na wengine kusombwa na maji, kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Akithibitisha vifo hivyo, Kamanda wa polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroard Mutafungwa, alisema watu wanne wa familia moja
walifariki dunia kwa kuangukiwa na ukuta wa nyumba walipokuwa wamelala huku wengine saba wakisombwa na maji ya mvua.
Kamanda Mutafungwa alisema tukio la kwanza lilitokea Mei 15 saa 7 usiku, katika maeneo ya Kijiji cha Konde tarafa ya Matombo Wilaya ya Mkoa wa Morogoro, ambapo watu wanne wa familia moja walifariki dunia kwa kudondokewa na ukuta wa nyumba yao wakiwa
wamelala kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Aliwataja marehemu hao kuwa ni Godfrey Augustin (35), Joyce Claud (38), Mariana Godfrey (10) mwanafunzi wa Shule ya Msingi Konde na
Senorino Godfrey (5) wote wakazi wa kijiji cha Konde.
Alisema watu wengine saba wakiwemo watoto watano walifariki dunia kwa
kusombwa na maji yaliyotokana na mvua kubwa iliyonyesha maeneo ya milimani na kusababisha maji mengi kuporomoka na kuingia
kwenye nyumba zao wakati wamelala usiku wa saa 8, huko katika kijiji
na kata ya Pemba tarafa na Wilaya ya Mvomero mkoani hapa.
Mutafungwa alisema watu hao waliofariki ni Peter Ferdnand (66), Tumbo John (37), Kauva Peter (35), Jack Tumbo (6), Kadudu Fikiri (9), Madi
Fikiri (14) na Mtupe John (8), wote wakiwa ni wakazi wa kijiji cha Pemba.
Aidha Mtafungwa alisema kuwa katika tukio hilo mtoto mchanga wa kiume wa marehemu Kauva Peter ambaye alikuwa bado hajapewa jina naye anahisiwa kufariki dunia, na kwamba mwili wake bado haujapatikana na
juhudi za kuutafuta bado zinaendelea.
Mutafungwa alisema miili ya Marehemu tayari imeshafanyiwa uchunguzi na daktari na kukabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya taratibu za
Mazishi.
Kamanda huyo pia aliwataka wananchi kuwa na tahadhari na mvua zinazoendelea kunyesha kwa kuepuka kuishi maeneo yaliyo karibu na njia za maji na kwenye nyumba za udongo.