23.6 C
Dar es Salaam
Friday, June 21, 2024

Contact us: [email protected]

Watoto Mwanza waiomba Serikali kuondoa shule maalum na kuimarisha ulinzi

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

Juni 16, 2024, Tanzania inaungana na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika. Wakati wa maandalizi ya maadhimisho haya, watoto mkoani Mwanza wameiomba Serikali kuondoa shule za wanafunzi wenye mahitaji maalum ili kupunguza unyanyapaa dhidi ya kundi hilo.

Pia wameiomba serikali kuimarisha ulinzi kutokana na vitendo vya kulawitiwa kwa watoto kuripotiwa mara kwa mara katika maeneo mbalimbali nchini.

Maombi hayo yalitolewa Juni 13, 2024, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika wilaya ya Ilemela, mkoani Mwanza, yakiandaliwa na Shirika la Fadhili Teens Tanzania (FTT) kupitia Mradi wa Msichana Thabiti.

Victoria Mathias na Nestory Amos waliiasa jamii, hasa wazazi, walezi, walimu na watumishi walioko katika madawati ya jinsia, kutunza siri za watoto wanaofanyiwa vitendo vya ukatili, hasa wanaolawitiwa au kubakwa. Walieleza kuwa baadhi ya wahanga wamekuwa wakiathiriwa zaidi baada ya siri zao kufichuliwa.

“Wengine wanalawitiwa lakini hawasemi kwa sababu hawawaamini hao wanaowaambia maana hawatunzi siri. Tunaomba wawe wanatunza siri za watoto ambao wamefanyiwa vitendo vya ukatili,” alisema Victoria.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa Chipukizi wa CCM Wilaya ya Ilemela, Iqra Amani, alisema: “Hata leo bado tunapambania haki zetu na uhai wetu. Vitendo vya ukatili wa kijinsia vimekuwa vikitushambulia sisi watoto, hasa wa Afrika. Vitendo kama vile kubakwa, kulawitiwa, kumwagiwa maji ya moto, na kunyimwa haki ya kucheza vinakatisha ndoto zetu,” amesema.

Mratibu wa Mradi wa Msichana Thabiti kutoka FTT, Sarah Emmanuel akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika.

Mratibu wa Mradi wa Msichana Thabiti kutoka Shirika la Fadhili Teens Tanzania (FTT), Sarah Emmanuel, alisema lengo la kuratibu maadhimisho hayo ni kuwaleta pamoja watoto ili waendelee kutambua haki zao za msingi, hususani masuala ya elimu na kuzuia ukatili wa kijinsia unaoendelea katika jamii.

“Natoa rai kwa walimu, wazazi, na walezi waendelee kutoa elimu bora na kuwafundisha watoto maadili mema hasa katika kipindi hiki ambacho taifa linaendelea na harakati za kutengeneza taifa lenye watoto walio na maadili, uelewa, na wanaotambua haki zao,” alisema Sarah.

Kwa mujibu wa Sarah, maadhimisho hayo yamewakutanisha watoto kutoka shule za sekondari na msingi Nyasaka pamoja na shule ya msingi Muungano zilizopo wilaya ya Ilemela, ambapo walifundishwa masuala mbalimbali yanayohusiana na maadili, elimu, na maarifa kutoka kwa afisa ustawi wa jamii, afisa elimu, polisi jamii, na Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) wa wilaya hiyo.

Tanzania ilianza kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka 1991. Lengo la maadhimisho hayo ni kuwaenzi watoto mashujaa takribani 2,000 wa kitongoji cha Soweto, Afrika Kusini, waliouliwa na askari wa utawala wa makaburu kwa ajili ya kudai haki yao ya kuendelezwa kielimu bila ubaguzi mwaka 1976. Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka huu ni “Elimu jumuishi kwa watoto izingatie maadili, maarifa, na stadi za kazi.”

Watoto wakiwa kwenye maandamano.
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles