|Asha Bani -Dar es Slaam
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umelaani kitendo cha kushikiliwa kwa Wakili Menrad D’Souza na wateja wake kwa amri ya Mkuu wa mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti juzi Julai 30, mwaka huu.
Mratibu wa Mtandao huo, Onesmo Olengurumwa amesema kitendo hicho ni ukandamizaji wa haki na uvunjwaji wa katiba ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Agosti Mosi, Jijini Dar es Salaam Olengurumwa amesema kuwa hawakufurahishwa na kitendo hicho hivyo wanalaani kwa nguvu zote na kuwataka wakuu wa mikoa na wilaya kufanya kazi kwa mujibu wa katiba.
“Wakili huyo alifungiwa katika chumba kwenye ofisi za Mkuu wa Mkoa Manyara juzi, kutokana na madai ya kushinikiza wakili na wateja wake waweze kuwasiliana na wakurugenzi wa wateja hao ili wakubali kuongeza kiasi cha fidia kwa wakulima katika mgogoro wa mbegu kati yao na wateja wa wakili D’Souza.
“THRDC kama mwavuli wa watetezi wa haki za binadamu inatambua kuwa mawakili ni watetezi wa haki za binadamu na wanafanya kazi zao za utetezi kwa mujibu wa sheria zilizowekwa na nchi,” amesema.