22.2 C
Dar es Salaam
Saturday, October 1, 2022

UPINZANI WASHANGILIA MATOKEO YASIYO RASMI ZIMBABWE

HARARE, ZIMBABWE


WAFUASI wa upinzani walikusanyika Makao Makuu ya Chama cha Movement Democratic Change (MDC), wakishangilia ushindi wa uchaguzi wa urais licha ya kwamba hakukuwa bado na matokeo rasmi.

Wafuasi hao walikuwa wakiimba na kucheza muziki kutoka katika spika zilizowekwa kwenye lori lililopo kwenye ofisi za MDC wakati chama hicho kikijumuisha matokeo.

Katika sehemu kubwa ya mji wa Harare, kulikuwa na utulivu, biashara na shughuli nyingine zikiendelea kama kawaida, huku watu wakijadili matokeo yasiyo rasmi yanayosambaa mitandaoni licha ya kuwa Tume ya Uchaguzi Zimbabwe (ZEC) ilikuwa bado kutoa matokeo ya awali.

ZEC ina siku tano za kutoa matokeo ya mwisho na imesema itatoa kwa wakati mwafaka. Ilitarajia kutoa ya awali jana jioni.

Hilo limekuja huku wagombea wote wakuu wakiwa na imani ya ushindi na kwamba wanachosubiri ni ZEC kutangaza mshindi.

Kiongozi wa MDC, Nelson Chamisa (40) alituma ujumbe kwenye mtandao wa Twitter akitangaza matokeo ya uchaguzi kutoka vituo zaidi ya 10,000 vya kura yameonyesha chama chake kimefanya vizuri.

Chamisa na Rais Emmerson Mnangagwa (75) ni washindani wakuu wa uchaguzi huo uliofanyika juzi, mara ya kwanza tangu mtawala wa muda mrefu Robert Mugabe aondolewe kwa mapinduzi yasiyo na umwagaji damu Novemba mwaka jana.

Mnangagwa, ambaye alichukua mamlaka baada ya kuondolewa kwa Mugabe, alisema anapokea taarifa ‘nzuri sana’ kuhusu kura za uchaguzi.

Hata hivyo, Mnangagwa, ambaye alieleza kufurahishwa na mwitikio mkubwa wa wapigakura, aliwataka watu wasubiri matangazo rasmi kutoka ZEC.

Makundi kadhaa ya asasi za kiraia yanakusanya matokeo kutoka vituo 10,985 vya kupiga kura sambamba na ZEC, lakini hayaruhusiwi kutoa matokeo kabla ya tume hiyo.

Chanzo kimoja cha habari kilisema ni mapema mno kumtangaza mshindi, lakini inaonekana kuna ushindani wa karibu sana.

Iwapo hakutakuwa na mgombea atakayepata zaidi ya asilimia 50 ya kura, duru la pili litafanyika Septamba 8, likishirikisha washindani wawili wa juu kati ya 23 waliowania urais.

Katika mji mkuu wa Harare, ngome ya chama cha MDC, matokeo yaliyowekwa nje ya baadhi ya vituo yalionyesha Chamisa akishinda kwa kura nyingi, lakini Mnangagwa alikuwa akitarajia kutamba  katika ngome za ZANU-PF za vijijini.

Kwa kawaida matokeo ya mjini hutokea haraka kuliko yale ya maeneo ya vijijini, ambako jamii ni masikini.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,373FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles