Hadija Omary, Lindi
Watumishi wa mamlaka za Serikali za Mitaa mkoani Lindi, wametakiwa kusimamia haki na upatikanaji wa kisheria kwa wananchi wanaowahudumia.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Januari 9, na mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa, Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali Watu, Dk. Bora Haule wakati akifungua mafunzo kwa watumishi wa serikali za mitaa yaliyowakutanisha wakuu wa Idara kutoka Halmashauri na wakuu wa vitengo wa sekretarieti ya mkoa kuhusu mradi wa kuboresha upatikanaji wa haki kwa wote hususani kwa wanawake.
Mafunzo hayo ambayo yatawafanya washiriki kwenda kutoa elimu kwa watumishi wenzao na wananchi juu ya haki za binadamu na hatimaye kusaidia kupunguza au kuondoa kabisa suala la uvunjifu na ukiukwaji wa haki unaosababishwa na wananchi au watumishi kwa kutokujua.
“Katika jamii kumekuwapo na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na upatikanaji wa haki kisheria kutokana na wananchi kutojua haki zao na wapi wanaweza kwenda kuzidai endapo zitakiukwa.
“Wananchi wanahitaji kuendelea kuelimishwa kuhusu masuala ya haki za binadamu na misingi ya utawala bora kwa kutumia njia mbalimbali ikiwamo ya vyombo vya habari,” amesema.
Naye mkurugenzi wa elimu kwa umma na mafunzo, Alexander Hassan aliupongeza mkoa kwa maamuzi ya kuanzisha kampeni ya kupambana na mimba za utotoni kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kupunguza kama sio kuondoa kabisa mimba kwa watoto.