|Safina Sarwatt, Moshi
Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Kilimanjaro, Emmanuel Mlaki amewataka wananchi wilayani hapa kutokuchagua viongozi kwa majaribio.
Aidha, amewataka kuwachagua viongozi CCM kwani ilani inayotekelezwa ni ya chama hicho, hivyo kuchagua viongozi upinzani ni kupoteza muda kutokana na kwamba hawana uwezo wa kutatua kero za wananchi.
Mlaki ameyasema hayo jana katika mkutano wa kampeni ya uchaguzi mdogo wa marudio ya udiwani wa Kata ya Mawenzi Mjini Moshi mkoani, Kilimanjaro.
“Vyama vya upinzani havina uwezo wa kuwaletea maendeleo wala kutatua kero za barabara, maji, wamachinga, bodaboda na bajaji, hivyo kuendelea kuwachagua ni kupoteza ndugu zangu msifanye majaribio kwa kuchangua viongozi kwani Chadema kwa sasa haina sera ndiyo maana kila kukicha tunarudia uchaguzi,” amesema Mlaki ambaye pia aliwahi kuwa Katibu wa Chadema Wilaya Moshi vijijini na Jimbo Vunjo, kabla ya kuhamia CCM.
Kwa upande wake mgombea udiwani wa Kata ya Mawenzi kupitia CCM, Apaikunda Naburi, ameahidi kutatua kero za wafanyabiashara wadogo wadogo, ili wapate maeneo ya uhakika ya kufanyia biashara zao bila kusumbuliwa.