Na Bakari Kimwanga-Dar es Salaam
MWALIMU Julius Nyerere, Rais wa kwanza wa Tanzania, alikuwa kiongozi mwenye maono. Alikuwa na wazo la wazi kabisa kuhusu aina ya jamii aliyotaka kuijenga nchini Tanzania.
Chini ya uongozi wake, mwaka 1967 Tanzania ilichukua rasmi Sera ya Ujamaa kama falsafa elekezi kwenye jitihada zake za kujiletea maendeleo. Lengo la serikali iliyoundwa baada ya ukoloni lilikuwa ni kujenga umoja, usawa na kuimarisha ushiriki wa wananchi kwenye harakati za kuleta maendeleo katika maeneo yao na Taifa kwa ujumla.
Mapema tu baada ya kupata uhuru mwanzoni mwa miaka ya 1960, mfumo wa elimu pia ulianza kufanyiwa mageuzi hatua kwa hatua ili kuendana na malengo hayo mapya ya Serikali.
Tangu miaka ya 1990 sera za Serikali zimekuwa zikiongozwa na ajenda za kiliberali za soko huria chini ya uongozi na msaada wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF). Mapema tu baada ya kupata uhuru mwanzoni mwa miaka ya 1960, mfumo wa elimu pia ulianza kufanyiwa mageuzi hatua kwa hatua ili kuendana na malengo haya mapya ya Serikali.
Kutokana na hali hiyo, hivi karibuni Shirika la HakiElimu lilizindua mpango mkakati wa miaka mitano kuanzia 2017-2021, ambapo pamoja na mambo mengine taarifa za watalaamu na mpango huo zimeainisha maeneo ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi kwa kina.
Profesa Kitila Mkumbo
Mhadhiri wa Chuo Kikuu kishiriki cha Elimu (DUCE) cha Chuo Kikuu Dar es Salaam, Profesa Kitila Mkumbo, anasema mfumo uliopo sasa unashindwa kuandaa vijana katika soko la ajira huku watalaamu waliopo vyuoni wakipewa kazi nyingine serikalini na nafasi zao zikiendelea kuwa wazi.
Anasema mfumo wa sasa wa elimu kuanzia ngazi ya msingi hadi chuo kikuu hauko vizuri ambapo kwa sasa elimu imebaki bila kuwa na njia mbadala ya kuiboresha zaidi ili kuweza kwenda sawa na mabadiliko ya dunia.
“Tunaposema elimu ni lazima tuandae ‘Global Citizen’ ambapo kwa sasa kitu hicho hatuna hapa kwetu. Sasa sekta ya elimu inakabiliwa na changamoto ya kiwango duni cha elimu inayotolewa, mfumo wa elimu hauwapi uelewa wahitimu na kwa upande wa elimu ya juu hawajajipanga vema.
“Wanaofundisha elimu ya juu wengi hawana sifa, ni robo tu ndio wenye sifa ya kufundisha na kati yao ni asilimia 41 tu ndio wenye PhD lakini wengine hawana.
“Tunahitaji wenye PhD wanaofundisha vyuoni angalau wafikie asilimia 60 na kuna haja ya kuishawishi Serikali kuwekeza katika elimu. Walimu ni tatizo kubwa, hivyo Serikali inatakiwa kuwaangalia na kuwapa mafunzo kwani ni muhimu mno na ni jambo endelevu,” anasema Prof. Mkumbo.
Kwa upande wake Dk. Joviter Katabaro anasema pamoja na hali hiyo, bado katika elimu yetu hakuna maandalizi ya kuwaandaa wahitimu kwenye soko la ajira.
Anasema ili kwenda sambamba na kasi hiyo, ni lazima kuwapo msukumo wa pamoja na somo maalumu la kuwandaa wahitimu pindi wanapomaliza masomo. Lengo ni kuweza kujiari hatimaye kupambana kikamilifu kwenye soko la ajira.
Mpango Mkakati wa HakiElimu
Akizungumzia mpango mkakati walionao, Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, John Kalage anasema wamelenga kushawishi mabadiliko ya sera kupitia ufumbuzi unaozingatia ushahidi, kufuatilia utekelezaji wa sera na kudai kutetea mageuzi.
Pia mkakati huo umelenga kukuza ushiriki wa jamii kupitia kuwapa taarifa wananchi, kutoa fursa ya kushiriki katika masuala ya kijamii na kukuza uwazi na uwajibikaji kwa kudai uwazi kwenye bajeti.
“Uwazi na uwajibikaji ni mambo muhimu katika utawala wa kidemokrasia, unawawezesha walipa kodi kutafiti na kujua kiurahisi utendaji wa Serikali, kuiwajibisha Serikali au viongozi wa kuchaguliwa kutokana na jinsi wanavyotumia fedha za walipa kodi kwenye ngazi zote,” anasema.
Akizungumzia shule tisa zilizofanya vibaya katika matokeo ya kidato cha pili Mtwara, anasema wazazi wanachangia wanafunzi kufeli.
Katika mpango mkakati huo, ilielezwa kuwa mambo yanayochangia kudorora kwa elimu ni pamoja na kupata matokeo duni ya ujifunzaji kwa wanafunzi, utoro wa walimu na umahiri duni wa kufundisha.
Uandikishaji waongezeka maradufu
Kalage anasema mafanikio makubwa yamepatikana kwenye kuongeza idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa shuleni ndani ya kipindi cha miaka 10 iliyopita. Ushahidi unaonesha kuwa uandikishaji umepanda kwa asilimia 26 kwa shule za msingi na sekondari.
Ongezeko kubwa zaidi limeshuhudiwa kwenye uandikishaji wanafunzi wa sekondari kwa asilimia 244 na udahili elimu ya juu kwa asilimia 438.
Gharama za elimu
Mkurugenzi huyo anasema mwenendo wa hivi karibuni wa bajeti ya elimu unaonesha umeendelea kubaki katika kiwango cha asilimia 21 ya bajeti ya Taifa.
Hata hivyo, mgawo wa sekta ya elimu kwenye bajeti ikiwa ni pamoja na kulipa madeni imebakia katika wastani wa asilimia 17, ikimaanisha kuwa kwa miaka kadhaa hakujawa na ongezeko kwenye eneo hili ikilinganishwa na bajeti ya Taifa.
Sera ya elimu 2014 na dhamira ya Serikali
Moja ya dhamira kubwa ya Serikali ni kutoa elimu ya msingi bure, kuinua ubora wa elimu kwa kuimarisha udhibiti ubora na ukaguzi wa shule, kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kama vile miundombinu ya shule, kutoa vifaa vya kujifunzia kwa usawa, na kuboresha utendaji wa walimu kwa kutoa mafunzo ya ualimu kazini na motisha.
Hata hivyo, anasema ili kufanikisha haya yote, serikali inahitaji kuongeza mgawo na kupeleka fedha na kusimamia utekelezaji wake kikamilifu.
Juhudi za Serikali na mafanikio
Anasema Tanzania imedhamiria kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 na imeandaa miongozo kadhaa ya kisera ili kutekeleza azma hii.
Changamoto za elimu
Licha ya juhudi za serikali zinazoendelea, sekta ya elimu nchini bado inakabiliwa na changamoto nyingi.
Kalage anazitaja baadhi ya changamoto hizo kama zilivyoanishwa kwenye Mpango Mkakati wa HakiElimu kuwa ni;
matokeo duni ya ujifunzaji kwa wanafunzi, utoro wa walimu na umahiri duni wa kufundisha.
Nyingine ni kukosekana kwa usawa wa kijinsia, kutojumuishwa kwa watoto wenye mahitaji maalum na mazingira magumu na ukatili uliokithiri shuleni.
Pia anataja kushamiri kwa mfumo-tabaka wa elimu ni kikwazo katika kuboresha elimu, ambapo anasema wenye fedha wachache wanamudu elimu bora kwenye shule binafsi na maskini wanaachwa kwenye elimu duni katika shule za serikali.
Kukosekana kwa falsafa na malengo ya elimu vinavyoeleweka kwa kila mtu nalo ni tatizo. Matokeo yake, elimu ya Tanzania imekosa falsafa na malengo ya kuiongoza.
Mabadiliko ya sera na utekelezaji wake
Mkurugenzi huyo anasema elimu ya Tanzania haina falsafa iliyo wazi na inashindwa kufikia ujumuishaji kamili wa makundi yote, imeshindwa kutoa matokeo bora ya kujifunza na yenye manufaa kwa wanafunzi.
Anasema wasichana bado ni waathirika wakubwa. Shule si sehemu salama, kwani mtoto mmoja kati ya wawili hukumbana na ukatili ambao umezoeleka kutendwa na walimu.
Hivyo kuna haja ya kufanyia marekebisho zaidi sera ya elimu na kampeni ya kuhimiza utekelezaji makini wa sera ya ya mwaka 2014 ili kuhakikisha upatikanaji wa elimu na ubora wake vinaimarika.
Hata hivyo, kushughulikia ukatili, kutengwa na kubaguliwa kwa baadhi ya watoto na masuala mengine kunahitaji mbinu na jitihada za pamoja kwa wadau mbalimbali na kuendelea kuutaarifu umma na kuhimiza mijadala ya umma.
Mpango mkakati wa HakiElimu 2017 – 2021
Anasema katika kipindi cha miaka mitano ijayo, lengo kuu litakuwa kufanya ushawishi kwa Serikali ili iandae na kutekeleza sera zinazozingatia ushahidi zitakazokuza fursa za watoto kuandikishwa shule, usawa na elimu jumuishi iliyo bora na inayotolewa kwenye mazingira rafiki na salama kwa wote.
“Mwishowe tunataka kuwa na mfumo wa elimu ulioboreshwa ambao unahimiza usawa, ujumuishaji na ujifunzaji wenye ufanisi.
“Huu utakuwa mfumo unaohimiza ufundishaji na ujifunzaji unaozingatia na kukuza usawa wa jinsia na kuwapo kwa mazingira rafiki ya kufundishia na kujifunzia,” anasema Kalage.
Ushiriki wa wananchi
Kiwango cha ushiriki wa wananchi katika sekta mbalimbali za kiutawala hapa nchini hasa kwa wanawake, kiko chini mno na bado kinashuka.
“Kwa mfano, ushiriki wa wananchi katika vikao vya kamati za shule ulipungua kutoka asilimia 36 mwaka 2006 hadi kufikia asilimia 15 mwaka 2013, hii ni sawa asilimia 13 ya kushuka kwa ushiriki wa wananchi kwenye huduma hii muhimu ya umma.
“Ni asilimia 22 tu ya wananchi hasa wanaume, huhudhuria mikutano ya mabaraza ya vijiji ambayo ni fursa muhimu kwa ajili ya kujadili masuala muhimu ya kijiji na kufanya uamuzi juu ya yanayoathiri watoto na elimu.
“Ni asilimia 16 tu ya wananchi ndio hushiriki katika kuandaa mipango ya kata na ya vijiji,” anasema.
Kutokana na hali hiyo, anasema idadi kubwa ya washiriki hawa ni wale waliopata elimu ya msingi tu, hii ina maana kuwa wasomi wengi kwa kiasi kikubwa hawashiriki michakato hii muhimu.
“Matokeo yake ni kwamba, ingawa kamati za shule, mikutano ya vijiji na kata ni fursa muhimu kwa ajili ya kufanya uamuzi unaoathiri watoto na elimu, kwa viwango hivi vidogo vya ushiriki wa wananchi, kuna uwezekano changamoto za sekta zitaendelea kubaki bila kutatuliwa.
“Ndiyo maana mkakati huu unataka kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa, wanajipanga na kushiriki kutatua matatizo muhimu, kufuatilia utawala na utoaji wa elimu bora.
“…tutajitahidi kufanikisha hili kwa kuhakikisha tunakuza na kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya elimu, jinsia na ukatili dhidi ya watoto. Tutahakikisha ushiriki wa wananchi na ufuatiliaji wa utawala wa shule na utoaji wa elimu bora unaboreshwa,” anasema.