32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wasiovaa maboya melini kuchukuliwa hatua

Nyemo Malecela -Kagera

SHIRIKA la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) mkoani Kagera limetangaza kuanza kuwachukulia hatua abiria wanaokataa kuvaa maboya wawapo safarini pamoja na manahodha wanaoshindwa kusimamia zoezi hilo.

Afisa Mfawidhi na Mkaguzi wa vyombo vya maji mkoani Kagera, David Chivagi alitoa tamko hilo jana kuwa kila abiria atakayekataa kuvaa boya atatozwa faini ya shilingi 500,000 wakati mmiliki wa chombo cha usafiri asiposimamia zoezi hilo chombo chake kitafungiwa kufanya shughuli ya usafirishaji ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani na kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela au vyote kwa pamoja.

Chivagi amesema changamoto kubwa ambayo wamekuwa wakikabiliana nayo ni abiria kutokubali kuvaa maboya huku manahodha wakiwa hawawaelekezi abiria kuvaa maboya hayo.

“Matokeo yake unakuta abiria wengine wameyalalia au kuyakalia badala ya kuyavaa kwa ajili ya usalama wao jambo linalosababisha yaharibike na kupoteza ubora.

“Tayari tumetoa elimu ya kutosha sasa kinachofuata ni faini ili fundisho katika jamii,” amesema Chivagi.

Chivagi alisema wakati mwingine manahodha na wasaidizi wake wanawaambia tu abiria kuwa; “boya hili hapa vaa, bila kuelekeza namna nzuri ya kulivaa, wapo wanao kataa kuyavaa kabisa wakidai wao ni magwiji katika kuogelea wakati ni kifo.”

Alieleza kuwa ajali ya hivi karibuni ya boti iliyokuwa imebeba abiria 56 pamoja na mizigo kuungua moto ikiwa inafanya safari katika Ziwa Victoria, abiria wengi walinusurika kutokana na uvaaji wa maboya.

Alisema wananchi na wamiliki wa vyombo vya usafiri wanapaswa kufuata sheria za usalama na ulinzi ikiwemo uhifadhi wa mazingira ikiwa ni pamoja na kutotupa vitu ovyo katika maji, kutochafua maji kwa kumwaga mafuta na kuzingatia usalama kwa watu walionao katika chombo

Alisema TASAC limepewa majukumu kadhaa ikiwemo kuhakikisha usalama wa vyombo vya majini, bandari na mazingira,  kuhakikisha nyaraka za mizigo inayoingia nchini na inayotoka ipo salama na zimekaguliwa lakini pia jukumu la kufanyia ukaguzi mizigo inayoingia na kutoka nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles