30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wasichana wafundwa wasihonge wanaume wakiamini wataolewa

CLARA MATIMO -MWANZA

IMEZOELEKA wanaume wengi ndio huwahonga wanawake fedha na vitu mbalimbali, lakini hali hiyo sasa imekuwa tofauti.

Wasichana wengi wanadaiwa kuwahonga wanaume, hasa wanapowadanganya  watawaoa.

Kuwapo wimbi hilo, inatajwa ni moja ya sababu zinazorudisha nyuma maendeleo yao kiuchumi kwa sababu fedha wanazozipata katika shughuli mbalimbali, badala ya kuzitumia kujiongezea kipato huishia mikononi mwa wanaume ambao baada ya muda huwaacha na kuoa wanawake wengine.

Hayo yalibainishwa jijini hapa juzi na Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Serikali la Wote Sawa linalotetea haki za mfanyakazi wa nyumbani na kupinga usafirishaji haramu wa mtoto, Angel Benedicto.

Alisema hayo wakati akizungumza na wasichana zaidi ya 50 katika mkutano mkuu wa tathmini ya mradi wa uwezeshaji shirikishi kwa wasichana wafanyakazi wa nyumbani uliolenga kuwawezesha kukua kiuchumi kwa kuwapatia mafunzo mbalimbali ya ujasiriamali.

“Hivi karibuni niliumia, kuna msichana mwenzenu mfanyakazi wa nyumbani  alidanganywa na kijana ambaye ni bodaboda, akamwambia atamuoa ila hajanunua vitu vya ndani, akamtaka kila mwezi akipokea mshahara awe anampelekea ili wafanye maandalizi… cha kusikitisha yule kijana baada kuchukua fedha miezi 10 mfululizo hakumtaka tena yule binti, alioa msichana mwingine, naomba hilo liwe somo kwenu.

“Acheni kuhonga wanaume, fedha zenu zitumieni kujiinua kiuchumi, tengeneza kesho yako leo, msijihusishe na mapenzi wakati bado mna umri mdogo, maana kati yenu mpo ambao mna miaka 16 na 17, hata mkipata ujauzito bila kutarajia bado hamjafikisha umri wa kujifungua uzazi salama, ambao ni kuanzia miaka 18 kwa mujibu wa wataalamu wa afya.

“Ukitafuta pesa ukawa na miradi yako, muda ukifika utampata mwanaume ambaye atakuoa kwa kufuata taratibu zinazotakiwa katika jamii zetu, hatakugeuza wewe mtaji, wale ambao bado mko kazini heshimuni waajiri wenu na kama hamfanyiwi ukatili msihamehame, mlioacha kazi, baada ya kupata mafunzo ya ujasiriamali mkajiajiri, heshimuni mitaji yenu msihonge wanaume,” alisema.

Ofisa Utetezi na Mawasiliano wa WoteSawa, Veronica Rodrick alisema mradi huo ulianza Januari, 2017 na umemalizika Desemba, mwaka huu na zaidi ya wasichana 100 wafanyakazi wa nyumbani wamenufaika na mafunzo ya kutengeneza vitu mbalimbali, ikiwamo  batiki, sabuni, vitafunwa na mapambo.

“Kwa kipindi cha miaka mitatu ya mradi tunashukuru tumeweza kuvunja umasikini kwa wanufaika, baadhi yao wameacha kazi za ndani ambapo walikuwa wanalipwa mshahara wa Sh 40,000, sasa wameajiriwa saluni wanalipwa Sh 150,000, wengine wamejiajiri na ambao bado wanafanya kazi waajiri wao wamewaruhusu kutengeneza bidhaa wanauza inawasaidia kuongeza kipato chao,” alisema Veronica.

Mwisho

Jamii ielimishwe mpango wa kutokomeza ukatili kwa wanawake, watoto – CSOs 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles