Mwandishi Wetu
KUNA kiwango kinafika mashabiki wa sanaa wanapenda kuona kazi zaidi zikiongea kuliko matukio ya wasanii sababu mengi huwa hayawahusu.
Msanii anaporuhusu kazi zake ziongee anakuwa na nafasi kubwa ya kudumu na kupata mafanikio kwa kuwa bidhaa yake (muziki,filamu nk) ndiyo inapewa kipaombele na mashabiki.
Msanii wa aina hii ndiyo wale ambao hata mabadiliko ya sanaa yakitokea huwezi kuona amepotea kizembe, vijana wapya wataibuka lakini yeye ataendelea kudumu kwenye nafasi za juu.
Jaribu kufuatilia mwenendo wa mastaa wakongwe kwenye muziki hata filamu pia utaona wengi wao ni wale ambao waliacha kazi zao siongee na siyo matukio mengine ambayo hayahusiani na sanaa.
Lakini hali imekuwa tofauti kwa asilimia kubwa ya wasanii wa kizazi hiki. Wameacha kufanya kazi na wamejikita katika kutengeneza matukio yatakayobusti kazi zao.
Mfano hivi karibu tumeshuhudia matukio mengi ambayo kimsingi hayana maana wala afya kwenye sanaa zaidi ya kutengeneza picha mbaya mbele ya jamii. Utaona mara wasanii wa kike wanaingia kwenye vita ya maneno lengo likiwa ni kuchafuana.
Ni kweli tunahitaji sanaa ichangamke lakini uchaguzi wa kipi kichangamshe gemu ni maamuzi ya wasanii wenyewe kwa kuzingatia hatma ya sanaa zao baada ya miaka kadhaa.
Tunahitaji wasanii wshindane kwenye kazi na sio kuingiza maisha yao binafsi kwenye tasnia. Inapendeza kuona wasanii wanashindana kujaza nyomi kwenye matamasha yao.
Mfano wiki hii, Ali Kiba yupo Kigoma, kwa mapokezi makubwa aliyopewa basi mashabiki wakaanza kuyashindanisha na yale aliyowahi kupewa Diamond Platnumz mkoani humo.
Huo ndio ushindani wenye tija unaotakiwa kwenye hii sanaa. Ushindani ambao unaongeza chachu ya wasanii kushindana kimafanikio na sio kushushiana heshima mbele ya jamii.
Sanaa yetu haihitaji ushindani unaodhalilisha utu na wewe shabiki una mchango mkubwa katika kukamilisha hili hivyo muda ndio huu. Wasanii shindaneni kwenye kazi na mashabiki sio vibaya kuwapuuza wasanii wanaoendekeza matukio kuliko kazi.