29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Jay R: Mtanzania kutoka Denmark mwenye ndoto za kumfikia Drake

COPENHAGEN, DENMARK

MUZIKI wa Hip hop umeendelea kuwavutia vijana wengi kutokana na uhuru unaowawezesha marapa kutoa mawazo yao kwa mitindo mbalimbali.

Miongoni mwa rapa hao ni Jason Mpesha ‘Jay R’ a.k.a Jason Raider, msanii Mtanzania anayeishi nchini Denmark ambapo leo amefanya mahojiano na Swaggaz ili shabiki upate kumjua zaidi kuhusu maisha na muziki, karibu.

Swaggaz: Jay R ni nani na lini ulianza kufanya sanaa yako ya muziki?

Jay R: Nimezaliwa mwaka 1999, Bukoba, Kagera. Nikiwa na miaka miwili baba yangu alifariki, sikuwahi kujua maisha yake ila nilisikia alikuwa daktari. Kiufupi alipofariki aliacha fedha na mali kwaajili ya kunisaidia mimi kwenye mambo ya shule na maisha.

Aliwaachia watu wa kusimamia hizo mali lakini walizitapanya, wakatumia kwa njia wanazojua wenyewe  na kufanya niishi maisha ya dhiki sana nikilelewa na babu yangu.

Mwaka 2004 babu alipofariki, kuna shule nilipelekwa nikawa nalipiwa kwa mashaka mashaka kwa sababu aliyepewa dhamana na  baba yangu alizitumia mwenyewe, ila maisha yangu ya shule na nyumbani yalikuwa ya dhiki tu maana hata walimu walikuwa wanajua naonewa.

Mwaka 2009, mama yangu alikuwa anaishi Ulaya ndio akaja kunichukua Tanzania nikaja kuishi huku na maisha yangu yakabadilika kwa kiasi fulani, nikaanza kwenda shule nzuri huku nikisisitizwa kusoma ili nije kuwa daktari kama baba yangu.

Baadaye nilipomaliza shule nilikuja Tanzania kwa mara ya mwisho kufuatilia mirathi ndipo niligundua mambo mengi sana na nikajifunza kwamba usitegemeee mirathi ikutoe kimaisha badala yake ufikirie unaweza kufanya nini wewe mwenyewe kupata mali.

Nilikuwa napenda kuja kuwa mtaalamu wa tiba mazoezi ila baadaye muziki ulikuwa kwenye damu tangu nikiwa na miaka 12 hivi nilianza kuandika nyimbo hapa hapa nyumbani Denmark. 

2018 niliachia wimbo wangu wa kwanza unaitwa Warrior, 2019 sikutoa wimbo kwa sababu nilikuwa mtu wa kukaa ndani (homeless) ila ni kipindi kilichonitengeneza kuwa mimi leo, niligundua maisha ni zaidi ya tunavyoishi, mwaka huu ndio nikaanza kuachia ngoma kibao.

Nimeachia EP moja inaitwa New Levels na Freestyle mbili, Why I Do This na nyingine inaitwa Am Turn Live inayopinga ubaguzi wa rangi kwa watu weusi na polisi wa USA wanavyowafanyia ‘Black Americans’.

Nikaachia ngoma nyingine inaitwa No Mercy na kwa mara ya kwanza nitaachia EP ya Kiswahili yenye ‘vibe’ za kina Wizkid, Davido, Diamond ili niweze kuifikia vizuri Afrika Mashariki maana huku Denmark ni ngumu kupata sapoti kwa Wadenmark, ninataka ‘nihiti’ dunia nzima na ili kufika kule lazima nipewe sapoti kubwa.

Swaggaz: Changamoto zipi unakutana nazo huko unapofanya muziki wako nje ya Afrika?

Jay R: Mashabiki wa huku wanapenda muziki wao kwahiyo ni tatizo sana kutoboa kwa sababu wanachagua sana, lazima uwaonyeshe kwamba unajua zaidi ndio wakupe sapoti, wanataka uwape sababu.

Swaggaz: Familia yako ina mchango wowote kwenye muziki unaofanya?

Jay R: Inanisapoti kwa kiasi chake, sababu bado inaamini kuwa natakiwa kuwa daktari na sio kufanya muziki.

Swaggaz: Kuna wasanii gani Tanzania unatamani kufanya nao kazi?

Jay R: Natamani sana kufanya kazi na Diamond, Harmonize, Rayvanny, Mbosso, Darassa, Fid Q, Marioo, Jux, Mr Blue na wengine ambao nimekuwa nikiwasikiliza tangu nikiwa mdogo.

Swaggaz: ‘Role model’ wako ni nani kwenye muziki wa Hip hop?

Jay R: Nilipokuwa nakua nilikuwa na ‘role model’ wengi, nilianza na Alikiba, Profesa Jay, Kala Jeremiah, Diamond Platnumz, Darassa, Jason Derulo, Tory Lanez na Drake.

Swaggaz: Una mipango ipo kwa sasa?

Jay R: Natoa albamu yangu fupi inaitwa Afro EP baada ya hapo kuna ngoma zitatoka za Hip hop ambazo nitazitoa zaidi mwaka huu kila mwezi.

Pia ningependa kuwashukuru mashabiki na kuwaambia waendelee kusapoti muziki wangu, wasapoti EP yangu ambayo itatoka siku ya birthday yangu Agosti 17, ina nyimbo nne ambazo ni Oh No, Angelina, Calling na Super Mama ambazo ni za Afro Pop.

Nawaambia mashabiki kuwa haya sio masihara, inakwenda kutokea kweli, nakwenda kufika kwenye levo za Drake na kuipa sifa Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles