33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

WAPAGAZI MLIMA KILIMANJARO WAANGALIWE

Na Upendo Mosha -Moshi

UNAPOZUNGUMZIA utalii hususani wa Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, huwezi kuwaacha mbali waongoza  watalii na wapagazi ambao wamekuwa kiungo kikubwa katika kuhakikisha wageni wanaofika nchini kwa lengo la kuupanda mlima huo wanafikia malengo.

Watu hawa wanaowaongoza watalii na wapagazi ambao wengi huzoea kuwaita wagumu, ni watu muhimu sana katika sekta ya utalii ambao huliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni.

Kundi hili ambalo limekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya utalii, limekuwa na kilio cha muda mrefu ambacho hakijasikika kwa makampuni wanayoyafanyia kazi na hata Serikali ambayo ndio mhimili wao mkuu.

Kilio kikubwa cha watu hawa ni masilahi duni ambayo wamekuwa wakidai yako kinyume na sheria na makubaliano waliyowekeana baina yao, makampuni ya kuhudumia watalii na Serikali.

Kimsingi ni kwamba muongoza watalii anapaswa kulipwa Dola za Marekani 20 kwa siku, huku wabeba mizigo wakipaswa kulipwa Dola 10 kwa siku, viwango ambavyo havitekelezwi, jambo ambalo limekuwa likiwafanya kufanya kazi katika mazingira magumu.

Watu hawa hupaswa kulipwa kwa dola lakini baadhi ya makampuni wamekuwa wakiwalipa kwa Shilingi bila kuthaminisha fedha hiyo  kutoka kwenye Dola za Marekani, hali ambayo husababisha wengi wao kulipwa fedha kiduchu ambazo hazikidhi.

Ni jambo la ajabu na kufedhehesha kwamba, mtu anapaswa kulipwa Dola 20 kwa siku lakini analipwa Sh 20,000, huku wanaopaswa kulipwa Dola 10 akilipwa Sh 10,000, fedha ambayo ni kidogo ikilinganishwa na stahiki wanazopaswa kulipwa.

Kilio  hiki ni cha muda mrefu kwa watu hawa, kwani mbali na masilahi duni, pia wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa vifaa ikiwemo vya kujikinga na baridi, hali ambayo imekuwa ikihatarisha usalama wa afya zao.

Kama tujuavyo hapa nchini yapo makampuni zaidi ya 200 ambayo yanahudumia watalii wanaopanda Mlima Kilimanjaro na Mlima Meru, lakini jambo la kusikitisha ni kwamba taarifa zilieleza kuwa kampuni ambazo zimekuwa zikiwahudumia vizuri wapagazi na waongoza watalii hazizidi tatu.

Taarifa hii ya kwamba kampuni za kuhudumia watalii zinazowahudumia vizuri kwa maana ya kuwalipa kwa kuzingatia misingi ya makubaliano wapagazi na waongoza watalii, hazizidi tatu na ni za kusikitisha kutokana na kwamba bila watu hawa, ni wazi kabisa kuwa utalii utazorota.

Ni ukweli usiopingika kwamba watu hawa wanaoitwa waongoza watalii na wapagazi, wana umuhimu katika sekta ya utalii hasa tukiuzungumzia Mlima Kilimanjaro na Meru, kwa kuwa hawa ndio husaidia kuwaongoza watalii na kuwabebea mizigo yao hadi kumaliza utalii wao hapa nchini.

Jambo hili ni la kutazamwa kwa jicho la tofauti, kutokana na kwamba yapo madhara mbalimbali ambayo yanaweza kutokea kutokana na tatizo hili la wapagazi na waongoza watalii.

Moja ya mambo ambayo yanaweza kujitokeza kutokana na tatizo hili ni baadhi ya wapagazi na waongoza watalii kutokuwa waaminifu na hata kijiingiza kwenye vitendo vya wizi ili kupata fedha za kujikimu wawapo mlimani na hata familia zao.

Tatizo la ukosefu wa uaminifu likizaliwa, linaweza kusababisha madhara makubwa katika sekta ya utalii, ikiwemo kuporomosha mapato yatokanayo na sekta hiyo kutokana na kwamba watalii wengi watahofia kufika nchini kwa ajili ya kupanda milima hiyo.

Jambo jingine ambalo linaweza kusababishwa na kuzaliwa kwa ukosefu wa uaminifu ni pamoja na kushuka kwa idadi ya watalii ambao wanafika nchini, kwa lengo la kupanda mlima Kilimanjaro na Meru na hivyo kuporomosha mapato yatokanayo na sekta ya utalii.

Ufike wakati sasa Serikali iliangalie suala hili na kulitafutia ufumbuzi wa kudumu, ili kuweza kuiimarisha sekta ya utalii nchini na kufanikisha malengo yaliyokusudiwa kupitia sekta hiyo.

Lakini lipo wazo ambalo limewahi kutolewa na Chama cha waongoza watalii la kuomba kuanzishwa kwa chombo kimoja kitakachowasimamia waongoza watalii na wapagazi, ni vyema Serikali ikalichambua wazo hili na kuona umuhimu wa kuunda chombo hicho.

Chombo kama hiki kitasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza malalamiko na ukandamizaji unaofanywa na kampuni zinazohudumia watalii nchini, kutokana na kwamba chombo hiki kitafuatilia kwa karibu na kuhakikisha wote wanalipwa haki zao kwa mujibu wa sheria.

Pamoja na kuundwa kwake ni vyema sheria zikawepo na kubainisha wazi, kampuni zitakazokiuka mikataba na kuwalipa wapagazi kiwango kisichokidhi ni hatua zipi watakazochukuliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles