21.5 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

UHIFADHI DUNI HUPOTEZA MAZAO YA NAFAKA

Na MWANDISHI WETU-

DAR ES SALAAM

MAZAO ya nafaka yakiwamo mahindi, mpunga, mtama na uwele ndio mazao makuu ya chakula ambayo hutumiwa na Watanzania wengi waishio maeneo ya mijini na vijijini.

Jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanywa na Serikali kuongeza tija kwa mazao hayo ambayo huhifadhiwa kwa muda mrefu zaidi kuliko mazao mengine ya chakula, ambapo uzalishaji wake umefikia wastani wa tani milioni 3,897,500 kwa mwaka.

Inaelezwa kuwa pamoja na ongezeko la uzalishaji, teknolojia zinazotumika katika uvunaji, utayarishaji na hifadhi ni duni na husababisha upotevu mkubwa wa mazao hayo, ambapo wastani wa tani 1559,000 za mazao ya nafaka  hupotea kila mwaka nchini.

Ili kukabiliana na changamoto hizo, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekamilisha kuandaa mkakati wa Taifa wa hifadhi ya mazao kwa lengo la kuwa na dira ya kupunguza upotevu unaojitokeza katika mazao ya chakula nchini.

Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya bajeti ya mapato na matumizi ya mwaka 2017/18, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tzeba, anasema Serikali imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto ya hali ya usalama wa chakula ikiwamo upotevu wa mazao kabla na baada ya mavuno na sumukuvu.

Anasema katika kuimarisha ubora na usalama wa mazao ya chakula nchini, Wizara kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (ASDP) II, itajenga makaushio ya kisasa 30 na kusambaza vifaa vya kukaushia kwa wakulima wa nafaka katika halmashauri za Sikonge, Chemba, Kondoa, Chamwino, Kiteto na Manispaa ya Dodoma kwa lengo la kudhibiti sumukuvu na madhara yake.

Anaongeza kuwa katika kuhakikisha mazao ya wakulima yanaongezewa thamani na kuwa na soko zuri, Wizara kupitia Programu ya ASDP II itajenga maghala manne yenye uwezo wa kuhifadhi tani 1,000 katika mikoa ya Singida (Mahindi), Mwanza (Mpunga), Kigoma (Mahindi) na Manyara (Mahindi).

Dk. Tizeba anasema Wizara itakamilisha ujenzi wa masoko na maghala 45 ya kimkakati katika mipaka ya Mulongo, Sirari, Kabanga, Kahama na Kyerwa-Nkwenda ili kuleta ufanisi katika biashara za mipakani na kudhibiti wafanyabiashara kutoka nje ya nchi kuingia moja kwa moja mashambani na kununua mazao ya wakulima kwa bei ndogo.

Kwa mujibu wa Dk. Tizeba, kupitia mradi wa kuongeza tija na uzalishaji wa mpunga, Serikali imekusudia kujenga maghala matano (5) yenye uwezo wa kuhifadhi tani 8,400 katika skimu za umwagiliaji za Njage (tani 1,700), Msolwa Ujamaa (tani 3,400), Mvumi (tani 1,300), Kigugu (tani 1,000) na Mbogo Komtonga (tani 1,000).

Aidha, Dk. Tizeba anasema Wizara kupitia Programu ya ASDP II itakamilisha ujenzi/ukarabati wa maghala 33 katika wilaya za Iringa, Njombe, Nsimbo, Mlele na Songea kwa ajili ya hifadhi ya mahindi, ambapo wakulima watahifadhi na kuuza mazao yao kwa pamoja na kujengewa uwezo kuhusu umuhimu na uendeshaji wa ushirika.

Kuhusu sumukuvu, anasema katika mwaka 2016/17 Serikali kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko imenunua tani 3,300.04 za mahindi kutoka kwa wakulima wa mikoa ya Iringa, Njombe na Ruvuma na kuongeza thamani ya zao kwa kusagisha tani 1,047.8 za mahindi.

Kupitia Programu ya ASDP imeweka vifaa vya kutunza ubora wa nafaka katika maghala 79 yanayohifadhi mahindi katika mikoa ya Rukwa–Halmashauri ya Kalambo (9), Ruvuma–Songea Vijijini (20), Songwe–Mbozi Vijijini (20), Mbeya–Mbeya Vijijini (13), Iringa–Mufindi (10), Njombe – Njombe Vijijini (7).

Akifafanua zaidi, Dk. Tizeba anasema katika kuongeza thamani ya mazao Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kupitia Mradi wa Sera na Maendeleo ya Rasilimali Watu, imenunua mashine 14 za kusindika mpunga katika skimu za Mombo Kivulini, Mawemairo, Ipatagwa, Ituro na Mbuyuni, Lekitatu, Mkula, Musa Mwinjanga, Nakahuga, Magozi, Kilangali, Mkindo na BIDP.

Waziri Tizeba anasema Wizara yake pia imefanya tathmini katika halmashauri za mikoa 12 ya Mwanza, Simiyu, Geita, Tabora, Kigoma, Shinyanga, Dodoma, Tanga, Morogoro, Kilombero, Arusha na ili kufahamu mahitaji ya ukarabati; ujenzi wa maghala mapya kwa ajili ya hifadhi ya mazao ya mpunga na mahindi.

Kuhusu sumukuvu, Dk. Tizeba anasema Serikali imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na tatizo hilo ikiwamo kuandaa andiko lililowasilishwa FAO na kupata ufadhili wa kudhibiti sumukuvu ambapo jumla ya Dola za Marekani 151,000 sawa na Sh milioni 300 zimetolewa na utekelezaji tayari umeanza.

Aidha, Serikali imelenga kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kupitia viwanda. Hata hivyo, ili kufikia malengo hayo ni lazima kuimarisha uzalishaji wa mazao ya kilimo ambayo ndiyo yatakuwa malighafi katika viwanda vinavyotarajiwa kujengwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles