26.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

WAKUU WA WILAYA HAWA WASIFUMBIWE MACHO

WAKATI Rais Dk. John Magufuli, anaingia madarakani, alitangaza wazi kabisa kuwa hakuna semina elekezi kwa wateule wake.

Uamuzi huo, ulipokewa kwa hisia tofauti na watu wa kada mbalimbali, kwa kuhoji iweje viongozi wasipewa semina elekezi kwa sababu miongoni mwao ni mara ya kwanza kuteuliwa kushika nyadhifa hizo.

Lakini pamoja na hisia hizo, hakuna mabadiliko yaliyotokea zaidi ya kuitwa Ikulu na kula kiapo mbela ya viongozi wakuu wa Serikali.

Baada ya kiapo hicho, kila kiongozi aliondoka kwenda sehemu yake ya kazi kama alivyoelekezwa. Lakini muda mfupi baadae tukaanza kushuhudia vituko.

Vituko hivyo ni pamoja na wakuu wa wilaya  kuagiza viongozi au watumishi wa umma kukamatwa na kuwekwa mahabusu.

Hatutaki kuelezea mlolongo mrefu, lakini tumelazimika kusema haya baada ya kutokea udhalilishaji mkubwa uliofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Gelasius Byakanwa anayedaiwa kukiuka maadili ya kazi.

DC huyo anadaiwa kumwamuru mwalimu wa Shule ya Sekondari Lerai, iliyopo Kata ya Bondeni, wilayani kupiga ‘pushapu’ mbele ya wanafunzi wake, jambo ambalo ni udhalilishaji.

Wakati huyo akifanya hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Chemba mkoa wa Dodoma, Simon Odunga naye anadaiwa kumpiga na kumjeruhi mkazi wa Kijiji cha Kambiyanyasa, Chindika Pingwa (57) kwa sababu mtoto anayedaiwa kuvunja kioo cha gari lake wakati wakicheza na wenzake.

Katika tukio la kwanza lilitokea Agosti 11, mwaka huu, baada ya mwalimu Erasto Mhagama kushindwa kujibu maswali aliyoulizwa na mkuu huyo wa wilaya.

Inaasikitisha kuona mkuu wa wilaya anajigeuza kuwa ofisa elimu kwa kufika shuleni na kuanza kuuliza maswali, si jambo baya inakuwaje anatoa adhabu?

Kitendo cha kumlazimisha mwalimu kupiga magoti tena mbele ya wanafunzi wake? hakikubaliki hata kidogo kwa sababu wale ni watoto ambao wanafundishwa na mwalimu wao kila siku.

Kwa kufanya hivyo ni kumjengea mazingira magumu mwalimu kukubalika mbele ya wanafunzi wake.

Tunapatwa na wasiwasi kwamba viongozi wengi walioteuliwa kushika nyadhifa hizi, ni wazi hawana elimu ya kutambua sheria na mipaka yao ya kazi zao.

Haiwezekani mteule wa Rais uliyeaminiwa unageuka kuwa mbogo kwa watumishi wa umma ambao masikini wa mungu wanashinda wana hangaika na watoto kila siku.

Katika hili tunaamini mamlaka zinazohusika haziwezi kumwacha DC huyu akaendelea kutamba kwenye nafasi hii, kwa sababu anaidhalilisha Serikali.

Pia tumesikitishwa na kitendo cha DC wa Chemba kumcharaza bakora mzazi wa mtoto eti kisa tu mwanaye amevunja kioo cha gari lake ambalo kimsingi ni mali ya Serikali.

Kutokana na matukio hayo mawili, tunaishauri mamlaka husika kuchukua hatua za kinidhamu  dhidi ya  viongozi hawa kwa sababu wamepoteza sifa ya kuongoza jamii.

Sisi MTANZANIA, tunaishauri mamlaka husika kuwapa semina elekezi kwa sababu viongozi wengi hawajui au hawatambui mipaka yao ya kazi.

Lakini pia tunaishauri Sekretarieti ya Madili ya Viongozi wa Umma kufanya kazi ya ziada ya kutoa elimu kwa wateule wa Rais ambao kwa namna moja au nyingine, wamekuwa wavunjifu wa amani katika jamii wanazoziongoza.

Tunasema hivyo, kwa sababu tume hii ina kazi kubwa ya kuwaelimisha viongozi hawa, ikiwa ni pamoja na kuacha tabia ya kutumia madaraka yao kukandamiza watumishi wenzao au jamii inayowazunguka.

Tunamalizia kwa kusema viongozi wa aina hii wanapaswa kujitafakari na kurudi kwenye mstari, badala ya kugeuka adui wa jamii wanayoingoza, ndiyo maana tunasema wasifumbiwe macho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles