HASSAN DAUDI NA MITANDAO
ONGEZEKO kubwa la idadi ya wanaume nchini China limewafanya wengi wao kuwa kwenye wakati mgumu linapokuja suala ya uhusiano wa kimapenzi.
Kufikia mwaka juzi, kulikuwa na ziada ya wanaume milioni 33 katika idadi ya wanawake waliokuwapo katika taifa hilo lenye watu wengi zaidi duniani.
Kwa mantiki hiyo, mwanamume anayesaka mpenzi au hata mke, hujikuta katika ushindani wa hali ya juu kutokana na uchache wa jinsia hiyo kwa sasa.
Wakiitumia hiyo kama fursa, baadhi ya wasomi wa masuala ya uhusiano wamejitosa kufungua shule zitakazowaokoa wanaume wanaokosa mbinu za kuwanasa wapenzi.
Wataalamu hao wamejihalalishia elimu hiyo kwa hoja kwamba kitendo cha wanaume wengi kuwa wapweke kinaweza kusababisha matukio ya kihalifu ikiwamo ubakaji.
“Wanaume wanapata shida, hasa wale wasio na fedha,” anasema Mwalimu wa Uhusiano, Li Yinhe.
Naye Yi Cui, mmoja kati ya wamiliki wa shule za aina hiyo, anasimulia namna anavyoendesha elimu hiyo ya kuwasaidia wanaume wenzake.
“Sehemu ya mafunzo wanayopewa wanaume wanapojiunga na shule hizo ni utanashati. Aina ya nguo za kuvaa, usafi wa nywele na mengineyo.
“Unajua hata wanaume walioingia katika uhusiano na wanawake, wengi hukimbiwa. Mara nyingi, huwa hawasafishi nywele na mavazi yao huwa si nadhifu.
“Pia kuna namna ya kusimama na mwanamke, hasa katika siku ya kwanza na aina ya maneno ya kumwambia,” anasema.
Msomi huyo anaongeza kuwa huwafundisha wanaume picha kali wanazotakiwa kuziweka katika mitandao ya kijamii ili kumvutia msichana.
Kuhusu gharama, anasema mwanafunzi atakayetaka kujifunza kutoka kwao kwa njia ya mtandao, atalipa Dola za Marekani 30 na yule atakayehitaji kuingia darasani kila siku, basi aandae Dola 4,500.
“Idadi kubwa ya wateja wake kwa sasa ni wanaume wenye umri wa miaka 23, yupo pia mwenye miaka 59, huku mdogo kabisa akiwa wa miaka 19,” anasema Cui.
Zhang Zhenxiao ambaye ni mkazi wa jijini Jinan, ni miongoni mwa wanaume walioamua kwenda darasani kujifunza namna ya kukabiliana na ushindani wa kupata mwenza.
Licha ya kuwa ana umri wa miaka 27 kwa sasa, hajawahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi, achilia mbali kupata walau mrembo wa kumtwanga busu.
Si kwamba hatamani kuwa na mwenza, bali kama ilivyo kwa wanaume wengine, angeanzia wapi kuumudu ushindani uliopo?
Mwalimu wake ni Zhang Mindong anayesema hata yeye alikuwa kama wanafunzi alionao sasa, akiwamo Zhang, yaani hakuweza kutongoza.
Mindong anasema hata alipoachana na mpezi wake mwaka 2012, aliumia mno kwa kuwa alijua wazi kazi imeanza upya, yaani ingemchukua muda mrefu kupata mwingine.
Akisimulia ilivyokuwa, anasema: “Nikaamua kujiunga na shule moja inayofundisha kutongoza ambayo iko chini ya wataalamu wawili; Cui Yihao (25) na Fan Long (29).
“Nakumbuka gharama za elimu hiyo zilikuwa zinatofautiana kutokana na mahitaji ya mwanafunzi. Kwa aliyetaka kusoma kwa njia ya mtandao, alilipa Dola za Marekani 45 (Sh 102,133).”
Anaweka wazi kuwa mwanafunzi ambaye angependa kuhudhuria vipindi vya darasani kwa kipindi chote, basi alikuwa akilipa Dola za Marekani 3,000 (zaidi ya Tsh milioni sita).
Juu ya elimu hiyo kukubalika na kuungwa mkono na wanaume wengi, Mindong anasema: “Takwimu za hivi karibuni juu ya elimu hii ya kufundisha wanaume kutongoza zinaonesha kuwa kumekuwa na mwitikio mkubwa kwa wanaume kwani waliojiunga wamefikia 300.”
Wakati huo huo, anajivunia mafanikio makubwa ya elimu inayotolewa na shule yake, akisema asilimia 90 ya wahitimu wake hurudisha majibu shuleni wakisema wameshapata wapenzi