Na MALIMA LUBASHA- SERENGETI
Wakazi wanane wa vijiji vya Kibeyo wilayani Serengeti mkoani Mara, wamekamatwa na kufikishwa katika Mahakama ya Wilaya kwa tuhuma za kuingia ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kufanya vitendo vya ujangili.
Mwendesha Mashtaka wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Emmanuel Zumba, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Ismael Ngaile, aliwataja washtakiwa hao  ni Amos Chacha (22), Marwa Ghati (20) na Nyabare Chacha (18)  waliokamatwa Desemba 19, mwaka jana, huku wakiwa na vipande vitatu vya nyama kavu ya Swala Impala vyenye thamani ya Sh 858,000.
Wengine ni Mniko Gesaro (30), Silasi Silasi (30), Chacha Kibone (30) na James Thomas (20) ambao walikamatwa siku hiyo hiyo eneo la Borogonja ndani ya hifadhi hiyo.
Baada ya washtakiwa kusomewa mashtaka matatu yanayowakabili walikana kuingia ndani ya hifadhi kinyume cha sheria hivyo hakimu aliamuru warudishwe mahabusu hadi kesi itakapotajwa Januari 3,2017.
Katika hatu nyingine, mahakama hiyo ilimuhukumu Chacha Itembe(40) mkazi wa Kijiji cha Kibeyo Kata ya Kisangura Tarafa ya Rogoro kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela na kulipa faini ya Sh 200,000 baada kutiwa hatiani kwa kosa la kuingia ndani ya hifadhi bila kibali na kupatikana na silaha.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Ismael Ngaile, alisema ametoa adhabu hiyo baada ya mshtakiwa kukiri kosa mwenyewe hivyo kuirahisishia mahakama kutoa adhabu na kulipa faini ya Sh 100,000 kwa kila kosa.
Hakimu Ngaile, alisema kosa la kwanza la kuingia ndani ya hifadhi bila kibali kinyume na kifungu cha 21(1) na (2) sura ya 29 kifungu (1) namba 11 ya mwaka 2003 kifungo ni mwaka mmoja na faini ya Sh100,000 na kosa la pili la kupatikana na silaha kisu , nyaya 3 za kunasia wanyama hifadhini kinyume na kifungu namba 24(1) (b) na (2).