DERICK MILTON -SIMIYU
HAKIMU wa Mahakama ya Mwanzo katika Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, aliyejulikana kwa jina la Jane Jewe amelalamikiwa na wananchi wa kata hiyo wakimtuhumu kuvurugha kesi zao, rushwa na matumizi mabaya ya lugha.
Wananchi hao walieleza kuwa hakimu huyo amedumu muda mrefu katika mahakama hiyo, zaidi ya miaka 10 hivyo wametaka aondolewe na waletewe hakimu mwingine.
Wakizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa huo, Antony Mtaka na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa na Wilaya, wananchi hao walimtaka mkuu huyo wa mkoa kumwondoa hakimu huyo.
Mmoja wa wananchi hao, Luja Masala akizungumza kwa uchungu mbele ya viongozi hao, alisema hakimu huyo ameshindwa kuendesha kesi yake kutokana na kushindwa kumpatia Sh 30,000 alichoombwa na hakimu huyo.
Masala alisema alikuwa na kesi ya wizi mahakamani hapo, ambapo alikuwa akimshitaki mmoja wa watu ambaye alikuwa jambazi sugu kijijini hapo baada ya kumwibia kiasi Sh milioni moja pamoja na nguo zake zote nyumbani kwake.
Alisema kuwa mtuhumiwa huyo, alikamatwa vizuri na askari polisi Kata ya Nkololo na baada ya kuhojiwa alikiri kumvamia na kumwibia kiasi hicho cha fedha polisi ndipo kesi yao ikafikishwa mahakamani hapo.
“Askari walifanya kazi yao vizuri na vielelezo vyote na kufikisha mahakamani, lakini baada ya kufika mahakamani hapo hakimu aliniomba 30,000 ili mtuhumiwa apelekwe katika gereza la Maswina lililoko Wilayani humo.
“Nilimwambia kuwa mimi sina na hapa nimeibiwa kiasi kikubwa, ndipo hakimu huyo alianza kunitukana na kusema kuwa najifanya mjuaji…na kueleza kuwa atanikomesha,”alisema Masala.
“Nilipokuwa nakwenda mahakamani, hakimu alikuwa akiniuliza kama nimekutana na mtuhumiwa wangu huko kijijini. Swali ambalo nilishindwa kulielewa,”alisema Masala.
Alisema licha ya kufikisha jambo hilo kwa uongozi wa Mahakama ya Wilaya kutaka asaidiwe na hakimu huyo kuandikiwa barua ya kutakiwa asikilize kesi yake, bado ilishindikana na hajui hatma ya kesi hiyo wala alipo mtuhumiwa.
Naye mkazi mwingine, Mboje Muhama alimwomba mkuu huyo wa mkoa kumwondoa hakimu huyo kwani amewanyanyasa vya kutosha.
“Kwenye mahakama yetu ya mwanzo tunakuomba mkuu wa mkoa, umwondoe hakimu huyu, hapa hakuna haki hata kidogo, wananchi tumemchoka tunaomba tuletewe hakimu mwingine, “alisema Muhama.
Akizungumzia kesi ya Masala, Kaimu Mkuu wa Kituo cha Polisi Nkololo, Ndobho Malima mbele ya mkutano huo alikiri jeshi hilo kumkamata mtuhumiwa huyo kisha kumfikisha mahakamani baada ya kumhoji.
“Anachoeleza mama hapo ni kweli, yule mtuhumiwa tulimkamata na kumhoji na alikiri kutenda kosa na tulikusanya ushahidi wote na kesi kuifikisha mahakamani kwa hakimu huyo,”alisema Malima.
Hata hivyo mkuu wa mkoa baada ya kuwasikiliza wananchi hao, alisema jambo hilo ni zito na litafanyiwa kazi na vyombo vya kiuchunguzi huku akihaidi malalamiko yao juu ya mahakama hiyo kuwa yatafanyiwa kazi na kila mmoja atapata haki yake.
“Naomba jambo hili nilichukue tukalifanyie kazi na vyombo vinavyohusika na kila mtu atapata haki yake,”alisema Mtaka.