Na FERDNANDA MBAMILA, DAR ES SALAAM
MTANDAO wa wanafunzi Tanzania (TSNP) umeitaka seriali kuufumua mfumo wa elimu nchini kwa vile umeghubikwa na mikakati hafifu katika harakati za kuikomboa elimu ya Tanzania.
Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Umoja huo kwa shule za sekondari.
Walisema licha ya jitihada nzuri za kuinua elimu nchini, mtandao huo kupitia idara yake ya utafiti na mafunzo unasikitishwa na mikakati hafifu ya Wizara ya Elimu katika harakati za kutibu bomu zito la mfumo wa elime nchini.
“Ikumbukwe kuwa Julai 20 mwaka huu TSNP ilipeleka mapendekezo wizarani kupitia waraka wake maalumu kuhusu muafaka wa taifa katika Mfumo wa Elimu Tanzania kwa Wizara ya Elimu 2016.’
“Lengo la waraka huu ni kuainisha sababu kuu mbili kati ya sababu nyingine zilizotolewa na wadau wengi wa elimu zilizosababisha mtandao wa wanafunzi Tanzania kuhubiri mapinduzi ya mfumo wa elimu Tanzania.
“Mfumo huu tulionao sasa tumeurithi kutoka kwa wakoloni , hivyo basi tungependa mfumo wa elimu urejee kitabu cha UJAMAA kilichoandikwa na hayati Mwalimu Nyerere katika kurasa za elimu ya kujitegemea.
“Mwalimu Nyerere alitilia shaka kuhusu mfumo wa elimu nchini na hoja kuu aliyoitoa ni ‘Urithi wa elimu ya kikoloni’.
“Alikiri kuwa hakukuwa na mkoloni ambaye alikuwa na dhamira au shabaha njema ya kumpa mwafrika elimu kuunda mfumo mpya wa elimu utakaoakisi mazingira yetu,” walisema.