Na Ramadhan Hassan,Dodoma
MSAJILI wa Baraza la Famasi Tanzania,Elizabeth Shekalaghe, imewapa onyo wamiliki wa maduka ya dawa za binadamu kuacha kuweka matangazo ya huduma katika milango ya maduka yao kwani ni kinyume na Sheria ya baraza hilo, huku akisema watakaokiuka watafungiwa kutoa huduma.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Desemba 10,2021,kuhusu matumizi holela ya dawa, ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kununua dawa kiholela kwani ni sumu na huleta madhara pale mtu anapotumia bila kufuata ushauri wa wataalamu.
“Kumekuwa na utaratibu watu kuweka mabango kwenye milango kana kwamba wanatoa matibabu au anaweka picha ya daktari kwamba tunatoa ushauri kama kuna huduma zinapatikana
“Niwaombe wamiliki wa maduka ya madawa kuacha mara moja na ndugu zangu nitakapopita na kukuta unatangaza, kisheria tunatakiwa kukufungia huduma,”amesema.
Aidha, amewataka wafamasia ambao hawajahuisha leseni zao kufanya hivyo kabla ya Desemba 31,2021 kupitia mfumo wa kielektroniki.
“Sheria inawataka wanataaluma wote kufanya marejeo ya leseni zetu kwa mwaka sasa hivi tupo katika hatua nzuri kwani kati ya wafamasia 2597 ambao wamesajiliwa 2479 wamehuisha leseni zao sawa na asilimia 93,”amesema.
“Ni vema wananchi mkafahamu kuwa zipo athari za matumizi yasiyo sahihi ya dawa na athari zake ni kuongezeka kwa ugonjwa,kutokupata nafuu,kutokupona na hatimaye kupelekea kifo,”amesema.
Amewataka wananchi kuepuka kununua dawa kwenye maduka ambayo hayajasajiliwa na Baraza la Famasi kwani ubora wake ni wa mashaka na maelezo juu ya dawa hizo yanaweza kupotoshwa.
Pia amewataka wafamasia,mafundi sanifu wa dawa na wasimamizi kuzingatia sheria.
“Wafamasia wenzangu tuhakikishe tunasimamia misingi ya utoaji huduma kwenye taaluma hii ambayo tumeisomea,”amesema.